Dili 3 zamwita Msuva Ulaya, za La Liga zimo

Muktasari:

  • Mshambuliaji wa Difaa El Jadida , Mtanzania Simon Msuva amepata ofa za kuondoka klabuni hapo kama tatu hivi, ikiwemo ya nchini Hispania lakini ametulia tu na kusisitiza hataki papara kwa sababu mambo mazuri hayataki haraka na sasa amewaachia waajiri wake suala hilo.

LICHA ya Mshambuliaji wa Difaa El Jadida, Saimon Msuva ‘Mane wa Morocco’ amekuwa na shauku ya kucheza soka la kulipwa Ulaya amesema hana papara ya ofa alizowekewa mezani na klabu kadhaa kutoka barani humo.

Msuva aliyefunga bao moja kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’, alisema kuondoka kwake Difaa kunategemea na maamuzi ya waajiri wake ambao ana mkataba nao unaomalizika 2020.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, aliipenyezea Nje ya Bongo kuwa miongoni mwa ofa walizonazo mezani ni kutoka kwa miongoni mwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.

“Kuna ofa kama tatu na miongoni mwa mataifa hayo ni Hispania, bado nina mkataba na Difaa kwa hiyo siwezi kusema ni timu zipi ambazo zimeonyesha nia ya kunihitaji.

“Ofa ya Hispania ni timu ambayo ipo Ligi Kuu. Difaa ndio wenye maamuzi ya mwisho ya wapi pa kuniuza ambako kutakuwa na maslahi kwao na kwangu, lakini binafsi natamani kucheza La Liga,” alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo alisema kinachomfanya kutamani kucheza soka la Hispania ni namna ya uchezaji ambayo haina tofauti sana na Morocco ambako wamekuwa wakicheza soka la kuvutia.

Aidha Msuva alisema kama itakuwa tofauti na matarajio yake haitakuwa sababu ya kumfanya ashindwe kwenda kwingine atakapopata nafasi kuonyesha makali yake.

“Tunachowaza wanadamu muda mwingine huenda tofauti maana yangu ni kwamba mipango sio matumizi. Kama nitaenda kwenye mataifa mengine nitahakikisha naendana na soka lao kwa muda mfupi kama ilivyokuwa Morocco,” alisema Msuva.