Difaa yamtumia tiketi Msuva juu kwa juu

Monday September 10 2018

 

By ELIYA SOLOMON

MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars, Saimon Msuva amepandishwa ndege juu kwa juu mwanangu na klabu yake ya Difaa El Jadida kurejea Morocco ili kuwahi mchezo wa robo fainali ya Kombe la Mfalme ‘Trone’ dhidi ya FAR Rabat.

Inshu nzima ya Msuva imeingiliwa kati na Rais wa Difaa El Jadida, Abdelatif Mouktarid ambaye alimpigia simu mshambuliaji huyo na kumuliza tiketi yake aliyokatiwa na TFF inaonyesha atarejea lini Morocco.

Msuva alimjibu rais huyo kuwa ni Jumatatu ya Septemba 11 na kwa mujibu wa mzunguko wa safari yake angetua Morocco, Jumanne.

Unaambiwa Mouktarid aligoma na kumweleza Msuva yeye ni mchezaji muhimu kwenye kikosi chao kwa hiyo anatakiwa kurejea mapema, muda mchache baadaye rais huyo akatuma tiketi.

“Badala ya kuondoka Jumatatu, nitasafiri Jumapili (jana) yaani wakati wenzangu wanarejea Tanzania, nitabaki hotelini ili saa tisa alasiri nipande ndege ya kwenda Morocco. Nitapitia Uturuki ambako nitabadili ndege ambayo itanifikisha Casablanca,” alisema mshambuliaji huyo.

Baada ya kutua Morocco, Msuva atajumuika na wenzake leo Jumatatu kwenye mazoezi ya jioni kabla ya kesho au kesho kutwa Jumatano kuelekea Rabat ambako watacheza mchezo huo kwenye Uwanja wa Mfalme Moulay Abdallah.

Difaa El Jadida anayoichezea Msuva ilitinga hatua hiyo ya robo fainali baada ya kuifunga Rachad Bernoussi kwenye hatua ya 16 bora kwa mabao 4-0.

Wakati huo huo, Mechi za kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ zimesogezwa mbele kufuatia kuendelea kwa michuano hiyo ya Kombe la Mfalme ambayo kwa Tanzania ni kama FA. Huu utakuwa msimu wa pili kwa Msuva kuichezea Difaa El Jadida ambayo alijiunga nayo msimu uliopita wa 2017/18 na kuifungia mabao 17, yakiwemo matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Advertisement