Dida ampa presha Manula Simba

Wednesday August 8 2018

 

By Thobias Sebastin

Dar es Salaam. Kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula, amesema ana kibarua kigumu cha kulinda kiwango chake katika mashindano ya msimu ujao.

Akizungumza Dar es Salaam, Manula alisema ana deni la kulipa kwa Simba na mkakati wake ni kucheza kwa kiwango bora ili kudhibiti nafasi yake.

Alisema ana wajibu wa kuonyesha ubora kwa kocha Patrick Aussems ili kuendelea kuwa kipa namba moja wa Simba na Taifa Stars.

Kipa huyo wa zamani wa Azam, alisema mafanikio aliyopata msimu uliopita ni makubwa, lakini ataongeza kasi kwenye mazoezi ili kulinda kiwango chake.

Pia alisema anatarajia kupata ushindani wa namba kwa kuwa Simba ina idadi kubwa ya makipa wakiwemo Deo Munishi ‘Dida’ na Said Mohammed ‘Nduda’.

“Nawaheshimu makipa wenzangu Nduda na Munishi walianza kucheza soka nikiwa nawaangalia si jambo dogo, leo tupo timu moja mimi nacheza wao wananisubiri,” alisema Manula.

Alisema uwepo wa Dida na Nduda ni changamoto kwake na ameahidi kutobweteka baada ya kupata mafanikio akiwa ndiye chaguo la kwanza kwa kocha wa makipa Muharami Mohammed ‘Shilton’.

Kocha Aussems amesema anatarajia kuwatumia makipa watatu msimu ujao Manula, Dida na Ally Salim aliokuwa nao kambini Uturuki, baada ya Nduda na Emmanuel Mseja kutokwenda na kikosi hicho nchini humo.

 

Advertisement