Diamond vs AliKiba : Hapa dunia itasimama tu

Muktasari:

Mwanaspoti linakuletea orodha ya ‘kolabo’ tano kubwa ambazo mashabiki wanazisubiri kwa hamu katika muziki wa Bongo Fleva.

BIFU kali lililokuwapo enzi hizo baina ya Haroun Rashid Kahena ‘Inspector Haroun’ na Juma Kassim ‘Nature’ lilifikia hatua watu kudhani kwamba, wawili hao hawawezi hata kutazamana usoni.

Inspector Haroun alikuwa akitisha kama njaa akiwa na kundi lake la Gangwe Mobb pamoja na Luteni Kalama, na ngoma yao ya ‘Mtoto wa Geti Kali’ iliwaweka juu.

Vita ya kuwania hadhi ya Mfalme wa Temeke ilipamba moto kati yake Inspector na Juma Nature a.k.a Kiroboto, aliyekuwa akikubalika kinyama uswahilini akitamba na ngoma kama ‘Hili Game’ na ‘Inaniuma Sana’.

Walipata makuzi ya pamoja kutokea udogoni na walikuwa pamoja hata wakati wakianza ‘gemu’ ya muziki, lakini umaarufu ukawatenganisha.

Utengano wao ulizaa bifu kubwa kiasi kwamba hakuna aliyetegemea kama wawili hao wangeweza kuja kukaa meza moja tena.

Lakini ‘remix’ ya wimbo ‘Mzee wa Busara’ ikawakutanisha wakongwe hao na urafiki wao umedumu tangu wakati huo.

Ilikuwa ni ‘kolabo’ kubwa iliyosubiriwa kwa hamu na hakika ilikata kiu za mashabiki wao.

“Mzee wa Busara akilia nyauuu, nyumba ya jirani watazika mtoto na watamsahau,” ulikuwa ni moja ya mistari mikali kutoka kwa Inspector katika ngoma hiyo iliyobamba ikilingana na matarajio ya mashabiki.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya ‘kolabo’ tano kubwa ambazo mashabiki wanazisubiri kwa hamu katika muziki wa Bongo Fleva.

ASLAY vs MBOSSO

Ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wanaunda kundi la Yamoto Band ambalo lilivunjika na sasa kila msanii amekuwa akipambana kivyake.

Aslay ndiye aliyekuwa msanii wa kwanza kuachia wimbo akiwa amesimama mwenyewe, ‘Angekuona’, kitendo kilichotafsiriwa kuwa mwanzo wa kuvunjika kundi hilo, baadaye akafuata Beka ambaye naye aliachia wimbo uliokwenda kwa jina la ‘Nibebe’ akisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuonesha uwezo binafsi.

Baada ya hapo Mbosso akajiunga katika lebo ya Wasafi (WCB) chini ya Naseeb Abdul ‘Diamond’ na tangu wakati huo amekuwa akifanya vizuri katika tasnia ya muziki.

Kama kuna kitu wadau wanasubiri kukiona ni Mbosso na Aslay kuimba wimbo wa pamoja au Yamoto wote kwa pamoja kuachia ngoma ya pamoja.

JOH MAKINI vs FID Q

Kwa miaka zaidi ya kumi wamekuwa wakicheza ligi ya peke yao kwenye muziki wa Hip Hop. Wakati fulani ilionekana Joh Makini ndio mkali wa Hip Hop na wakati mwingine ilionekana Fid Q ndiye mkali katika gamu hiyo.

Kila mmoja kati yao anaamini ndiye anayestahili taji la ufalme wa muziki huo. Hawajawahi kushuka tangu walipopanda mahali walipo. Joh Makini akitokea Arusha huku Fid Q akitokea Mwanza hatujui kama watakuja kufanya kolabo ila ni kitu kinachosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wao.

LADY JAYDEE vs MWANA FA

‘Alikufa kwa Ngoma’, ‘Hawajui’ na ‘Msiache Kuongea’, ni baadhi ya ngoma ambazo walifanya pamoja washikaji hawa wa zamani na kuiteka tasnia ya Bongo Fleva.

Upepo mbaya ulipita kati yao wakati Jaydee akijiandaa kuzindua albam yake ya ‘Anaconda’ mwaka 2013 huku MwanaFA akijiandaa kuzindua wimbo wake wa ‘Kama Zamani’ aliowashirikisha Mandojo na Domokaya na kundi la Kilimanjaro Band wana Njenje.

Tarehe ya uzinduzi ya MwanaFA ilifanana na ya uzinduzi wa Jaydee. Jide aliahirisha onyesho lake na FA pia aliahirisha kutokana na kifo cha msanii Mangwair na pia kifo cha rapa Langa Kileo. Na mara zote tarehe mpya za uzinduzi zikafanana. Jide alimtuhumu FA kuwa anatumiwa kumharibia onyesho lake.

Hatimaye wote wawili wakazindua siku moja FA akitumia ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Posta na Jide akitumia ukumbi wa Nyumbani Lounge. Bifu lilikuwa kali sana. Walipachikana majina mabaya huku mitandao ikishika kasi kwa malumbano baina ya pande mbili hizo.

Miaka minne baadaye, 2017, MwanaFA alionyesha kwamba bifu baina yao lilishamalizika akiposti katika ukurasa wake kusapoti video ya wimbo mpya wa Jide uliokuwa umetoka wakati huo wa ‘I Miss You’. Na tangu wakati huo mambo baina yao yanaonekana kuwa amani tupu. Kolabo yao inasubiriwa sana.

DIAMOND vs OMMY DIMPOZ

Walikuwa ni washakaji na walifanikiwa kutoa wimbo mmoja wakishirikiana na Victoria Kimani unaokwenda kwa jina la ‘Prokoto’ ambao ulifanya vizuri.

Baadaye wawili hao waliingia katika bifu zito lililofikia hata kukashifiana hadi wazazi wao baada ya Dimpoz kuweka picha ya mama mzazi wa Diamond na kuandika ujumbe kwamba yeye ni baba yake, kitendo ambacho kiliibua hisia za wadau wengi wakimtaka aondoe ujumbe huo kwani waliogombana ni wao hivyo wasiwahusishe wazazi.

Tangu wakati huo, Dimpoz ameonekana kuwa karibu zaidi na mpinzani wa Mondi, Ali Kiba na amekuwa akizua maswali kutokana na ‘kuelewana’ na wapenzi waliotengana na Mondi kama Wema Sepetu aliyemshirikisha katika video ya wimbo wake wa ‘Wanjera’, au ‘Zari the Boss Lady‘ aliyeonekana akipiga naye picha.

Ni suala la kusubiri kama wawili hawa wanaweza kufanya tena kolabo.

ALIKIBA vs DIAMOND

Zamani walikuwa ni washikaji, usingeweza kushangaa ukisikia Alikiba ndio alimpa ruhusa Bob Junior amsaidie Diamond kwenye studio ya Sharobaro Records. Ni kitu ambacho kilifungua njia nyingi kwa Diamond. Pengine bila uungwana wa Kiba tungechelewa kumfahamu Diamond.

Ilikuwa habari kubwa wakati fulani pale ilipovuja kuwa Diamond alifuta sauti ya Kiba kwenye wimbo wake wa ‘Lala Salama’ huku Kiba pia akigoma kufanya kolabo na Diamond kwenye wimbo wake wa ‘Single Boy’ ambao ulihitaji watu wawili.

Kiba na Diamond wametengeneza ligi kwenye Bongo Fleva kuanzia redioni, kwenye runinga mpaka kwenye mitandao ya kijamii na ndio wasanii wanaoaminika kuwa na mashabiki wengi zaidi nchini kwa sasa. Mvutano ulidaiwa kuwafanya wawili hao kushindwa hata kupeana mikono walipokutana.

Ukubwa wa vipaji vyao, wingi wa mashabiki wao na picha ya uhasama baina yao iliyojijenga vichwani mwa watu, inabashiriwa kwamba siku wakiweka silaha chini na kuamua kupiga pesa, itakuwa ni moja ya kolabo za kihistoria katika muziki wa kizazi kipya. Nchi itasimama.