Diamond, Rayvan wafungiwa muda usiojulikana

Muktasari:

Tamasha la Wasafi lilianza kufanyika wiki kadhaa zilizopita ambapo kwa mara ya kwanza lilifanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara chini ya uongozi wa Diamond.

Dar es Salaam. Kisa wimbo wa Mwanza, Wanamuziki, Nasib Abdul (Diamond Platinumz) na Raymond Mwakyusa (Rayvan) wamefungiwa kufanya matamasha ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana kuanzia Leo Desemba 18, 2018.
Wanamuziki hao wamefungiwa na BASATA kwa kile ilichodai ni utovu wa nidhamu kwa Mamlaka zinazosimamia masuala ya sanaa nchini na uvunjifu wa maadili.
Taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa leo Desemba 18, imesema limefikia uamuzi huo baada ya wasanii hao kuonyesha dharau kwa mamlaka zinazosimamia shughuli za sanaa nchini, kwa kufanya vitendo vinavyokiuka maadili.
Mbali na kuwafungia wanamuziki hao, Baraza limetangaza kukifuta kibali cha Tamasha la Wasafi Festival linaloendelea nchini.
Wimbo wa Mwanza ambao uliowaingiza matatani ulifungiwa Novemba 12.
Juzi, Basata iliahidi kutoa taarifa rasmi baada ya wasanii hao kuonekana jukwaani katika Tamasha la Wasafi jijini Mwanza wakitumbuiza wimbo huo.
Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Onesmo Kayanda alisema Baraza limefikia uamuzi huo kutokana na wasanii hao kuendelea kuonyesha utovu wa nidhamu.
"Itakumbukwa kwamba Novemba 12, Baraza lilifungia wimbo wa Mwanza wa wasanii hao, lakini bado wameendelea kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu," alisema Kayanda.