Deschamps ampeleka Pogba kwa Real Madrid

Muktasari:

  • Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane anafahamika wazi kuhitaji huduma ya kiungo Pogba katika kikosi chake

Paris, Ufaransa. Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps yupo tayari kumsaidia kiungo wa Manchester United, Paul Pogba kwenye mpango wa kutimkia Real Madrid katika dirisha dili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Pogba ambaye Deschamps amemtaja kwenye kikosi chake cha Ufaransa kitakachocheza mechi mbili za kufuzu Euro 2020, amekuwa akihusishwa sana na mpango wa kutimkia Bernabeu.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane anafahamika wazi kuhitaji huduma ya kiungo huyo huku mchezaji mwenyewe akiwahi kukiri kwenda kucheza Bernabeu ni ndoto yake kubwa.

Siku za karibuni Pogba amekuwa akicheza chini ya kiwango, lakini jambo hilo halijawahi kuwa tatizo kwa Deschamps na kuamua kumjumuisha katika kikosi chake kwanza kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Bolivia kisha kufuatia mechi za kufuzu Euro 2020 dhidi ya Uturuki na Andorra mwezi ujao.

Deschamps alisema: "Kushuka kiwango si kitu cha Paul peke yake. Kama utaniuliza kuhusu kuhamia Real Madrid, basi nitampa ushauri wangu."

Kocha Deschamps ameendelea kuwa na imani kwa Pogba licha ya kuwapiga chini mastaa kibao wa Ligi Kuu England kwenye kikosi chake akiwamo straika wa Alexandre Lacazette, beki wa Manchester City, Aymeric Laporte na fowadi wa Man United, Anthony Martial, ambao wote hajawachagua.

Kikosi cha Ufaransa, makipa: Hugo Lloris (Tottenham), Benjamin Lecomte (Montpellier), Alphonse Areola (PSG), Mike Maignan (Lille)

Mabeki: Ferland Mendy (Lyon), Lucas Digne (Everton), Clement Lenglet (Barcelona), Samuel Umtiti (Barcelona), Raphael Varane (Real Madrid), Kurt Zouma (Everton/Chelsea), Leo Dubois (Lyon), Benjamin Pavard (Bayern Munich)

Viungo: Paul Pogba (Man United), Tanguy Ndombele (Lyon), N’Golo Kante (Chelsea), Blaise Matuidi (Juventus), Moussa Sissoko (Tottenham)

Washambuliaji: Olivier Giroud (Chelsea), Kylian Mbappe (PSG), Kingsley Coman (Bayern Munich), Antoine Griezmann (Atletico Madrid), Florian Thauvin (Marseille), Wissam Ben Yedder (Sevilla), Thomas Lemar (Atletico Madrid).