Dembele ni pasua kichwa

BARCELONA HISPANIA. OUSMANE Dembele amejiweka kwenye matatizo makubwa huko Barcelona baada ya kuchelewa tena mazoezini.

Staa huyo Mfaransa amekuwa akiandamwa na matukio mbalimbali ya utovu wa nidhamu tangu alipotua Nou Camp.

Staa huyo alichelewa kwa dakika 15 kwenye mazoezi ya timu yake ya Jumatatu iliyopita.

Kwa mujibu wa Marca, ameingia kwenye kumbukumbu mbaya za klabu hiyo. Dembele aliwasili kwenye kambi ya mazoezi ya klabu hiyo huko Ciutat Esportiva Joan Gamper asubuhi ya saa 4:15 Jumatatu iliyopita.

Hiyo ilikuwa ni dakika 15 zaidi ya muda ambao Kocha Ronald Koeman alisema ni mwisho wachezaji wake wote wanapaswa kuwa wamefika mazoezini.

Kocha huyo Mdachi alihitaji wachezaji wake wawasili walau saa moja kabla ya kuanza kwa mazoezi. Hata hivyo, hii ni mara ya kwanza kwa Dembele kuchelewa mazoezini tangu Koeman alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo kitu ambacho anaweza kuchukuliwa hatua kali za kinidhani.

Mwaka 2018, staa huyo aliyesajiliwa kwa ada ya Pauni 124 milioni alikuwa na kawaida ya kuchelewa vikao vya timu na mazoezini.

Kuna wakati, staa huyo alichelewa kwa saa mbili, alipigwa faini ya Pauni 90,000.

Dembele aliwekwa benchi kwenye kikosi cha Barcelona kilichoichapa Villarreal 4-0 kwenye mchezo wa La Liga Jumapili iliyopita.

Ansu Fati, Philippe Coutinho na Antoine Griezmann walimsaidia Lionel Messi kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, huku Fati akifunga mara mbili kwenye dakika 20 za mwanzo kabla ya kutolewa na Dembele kuingia dakika 20 za mwisho. Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Dembele tangu Novemba mwaka jana.

Ripoti zinadai Manchester United sasa inapiga hesabu za kwenda kumsajili staa huyo wa zamani wa Borussia Dortmund baada ya kuona mipango yao ya kunasa saini ya Jadon Sancho kuzidi kuwa ngumu.