Dele kuchomolewa kwenye domo la Jose Mourinho

Wednesday September 30 2020

 

 PARIS, UFARANSA. MABINGWA wa soka wa Ufaransa, Paris Saint-Germain ipo tayari kumpa Dele Alli njia ya kutorokea baada ya kukumbana na wakati mgumu kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur kwa sasa.

Dele Alli hana uhusiano mzuri na kocha wake Jose Mourinho huko kwenye kikosi cha Spurs na PSG wanataka kumsajili Mwingereza huyo kwa mkopo kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa.

Mabingwa hao wa Ufaransa wamedai kwamba watafikiria kumsajili jumla staa huyo ili kumwondoa kwenye tatizo la Mourinho jumla. Dele Allia anaonekana kuwa tayari kuondoka baada ya kuwekwa benchi tu kwenye mechi mbili za ligi zilizopita.

Ripoti zinadai kwamba mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy anafikiria kukubaliana na dili hilo. Timu hizo zimekuwa na uhusiano mzuri, ambapo PSG iliwauzia Spurs wachezaji wawili, Lucas Moura na Serge Aurier katika miaka ya karibuni.

Alipoulizwa kuhusu Dele Alli kukaa benchi, Mourinho alisema: “Kuna wengine pia wanasubiri kucheza. Haya ni mapambano ya ndani, mapambano baina ya marafiki. Kila mtu atapata nafasi ya kucheza.”

Na alipoulizwa kama Dele Alli atabaki Spurs hata baada ya dirisha kufungwa, Mourinho alisema: “Naamini hivyo.”

Advertisement

 

 

 

Advertisement