Dele Alli noma, kammwaga demu wake kisha kabeba mwingine

Muktasari:

  • Dele Alli aliamua kumtema mrembo wa mitindo, Ruby, mwenye umri wa miaka 23, wiki tatu zilizopita.

LONDON, ENGLAND . MADEMU wakali waliokuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, mmoja wao alikuwa mrembo Ruby Mae.

Ukiweka kando fainali hizo zilizofanyika Russia, mrembo huyo alikuwapo pia kwenye fainali za Euro 2016 zilizofanyika Ufaransa. Si kwamba anapenda sana soka, bali kuna mtu mmoja alikuwa akimfanya apige safari zote hizo. Dele Alli.

Kipindi hicho, mrembo Ruby alikuwa hasikii wala haoni juu ya mapenzi tele kwa supastaa huyo wa kimataifa wa England, anayekipiga kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur.

Lakini sasa kufumba na kufumbua, Dele Alli amemwaga Ruby. Mbaya zaidi hata mwezi haujafika tangu bibie Ruby amwagwe, tayari Dele Alli ameshaong’oa kifaa kipya. Macho ya staa huyo wa Spurs kwa sasa yameangukia kwa mrembo, Megan Barton Hanson.

Dele Alli aliamua kumtema mrembo wa mitindo, Ruby, mwenye umri wa miaka 23, wiki tatu zilizopita.

Mrembo Ruby hakutaka kulipoteza penzi la Dele Alli na alipambana sana, lakini kwenye akili ya mwanasoka huyo tayari mambo yalikuwa yameshafikiwa uamuzi kwamba, basi hataki tena.

Dele, 22, aliwaambia marafiki zake wa karibu baada ya kudumu kwenye uhusiano wa kimapenzi na mrembo Ruby kwa miaka miwili na nusu, kwa sasa anataka kufurahia maisha tena akiwa singo. Hataki kubanwa wala kujikaba.

Lakini wakati akiwaambia wenzake anataka kuwa singo, siku chache tu, anakutana na mrembo Megan, 24, ambaye naye yupo singo, wakabadilishana namba na kilichofuatia baada ya hapo, wanakifahamu wenyewe. Wawili hao walikutana Jumamosi iliyopita kwenye klabu moja ya usiku huko London.

Kuna mtu mmoja alisema hivi: “Dele alimwambia Ruby mambo hayaendi tena. Ruby alihuzunika sana akipambana wabaki kuwa pamoja, lakini akili ya Dele ilishaamua.

“Haikuchukua muda mrefu na sasa anafurahia maisha yake akiwa singo, akienda kuponda raha na huko ndiko alikokutana na Megan kwa mara ya kwanza.”

Mrembo Megan aliachana na staa mwenzake wa Love Island, Wes Nelson, mwezi uliopita tu hapo. Megan alimshutumu mrembo Vanessa Bauer ambaye ni patna wa mpenzi wake Nelson kwenye mashindano ya kudansi kuwa ndiye chanzo cha kuachana kwao.

Siku ambayo Megan alikutana na Dele Alli alipigilia kivazi matata kabisa, kigauni cha mpira rangi ya pinki kilichouchora mwili wake kisawasawa, kiasi cha kumfanya staa huyo wa soka ashindwe kuvumilia.

Dele alikuwa na marafiki wake kibao kwenye eneo hilo, akikwepa kupigwa picha. Baada ya muda tu, staa huyo alifanya uamuzi.

“Dele alimwelewa Megan na alimfuata moja kwa moja kujitambulisha. Kulikuwa na mademu wengine wakali sana, mastaa wenzake Megan, lakini macho ya Dele yaliangukia kwa Megan tu.

“Akamwambia amependeza na ni mrembo pia kabla ya kumwomba amtoe kwa ajili ya chakula cha usiku siku nyingine. Muda mfupi baadaye, wakapeana namba za simu,” alisimuliwa mmoja wa waliokuwa kwenye ukumbu huo wa starehe za usiku na kuongeza.

“Megan alipagawa. Alitulia kwa mshangao na akamwona Dele ndio saizi yake kabisa kuweza kutoka naye. Aliulizauliza maswali, akitaka kufahamu kama kweli ameshamwagana na mrembo Ruby.”

Wakati hayo ya Dele Alli na mrembo Megan yakiendelea ndani ya kumbi hiyo ya starehe, huko nje usiku huo huo kuliripotiwa watu watatu kuchomwa vitu vyenye ncha kali.

Dele kwa sasa ni majeruhi ingawaje inadaiwa anaweza kurejea uwanjani fasta, aliukosa mchezo wa Spurs wakati iliposhinda Tatu Bila dhidi ya Borussia Dortmund kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.