Dean, refa mtata kapewa kazi Man United vs Arsenal

MANCHESTER, ENGLAND. MPO? Mike Dean ametajwa kuwa mwamuzi wa mchezo wa Manchester United dhidi ya Arsenal utakaopigwa Jumapili uwanjani Old Trafford.

Hata hivyo, uteuzi huo wa Ligi Kuu England haujachukuliwa vyema baada ya mashabiki wa timu zote mbili kubaki na wasiwasi mkubwa kabla ya mchezo wenyewe kwenda kufanyika.

Dean, 52, amechukulia umaarufu mkubwa kutokana na aina yake ya uamuzi anavyofanya anapokuwa kwenye mechi.

Dean amechezesha mechi nyingi kuliko mwamuzi yeyote, akichezesha mechi 513, wakati anayefuatia amechezesha mechi 415, ameonyesha kadi nyekundu 105, anayefuatia ameonyesha kadi 67 na ametoa penalti 173, anayefuatia penalti 96, akifunika kwenye vipengele vingi kuliko vya waamuzi wengine wote kwenye historia ya Ligi Kuu England. Mashabiki wa Arsenal pia wameonyesha wasiwasi wao juu ya Dean na rekodi yake ya penalti ambazo amekuwa akiwapa Man United.

Man United imepewa penalti 36 kwenye michuano yote tangu ilipoanza kunolewa na Ole Gunnar Solskjaer. Rekodi zinaonyesha kwamba Man United imeibuka na ushindi kwenye mechi 40 na kupewa penalti 18 katika mechi 74 ilizocheza mwamuzi akiwa Dean, huku Arsenal wao wakishinda mara 36 na kupewa penalti sita tu katika mechi zao 75 alizochezesha mwamuzi huyo.

Timu hizo mbili zote kila moja imewahi kuonyeshwa kadi sita nyekundu na mwamuzi Dean, ambaye aliwahi kuchezesha mechi sita za Ligi Kuu England baina ya miamba hiyo. Katika mechi hizo sita za Arsenal dhidi ya Man United ambazo mwamuzi alikuwa Dean, mechi mbili zilizomalizika kwa sare, huku Man United ikishinda nyingine nne zilizobaki na wamepata penalti mbili kwenye ushindi huo. Kiungo, Jack Wilshere alikuwa mmoja wa wachezaji waliotolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Dean katika mechi za Man United na Arsenal.

Baada ya uteuzi huo wa mwamuzi Dean kuchezesha mechi hiyo, mashabiki wa Arsebal wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kutoa maoni yao, ambapo shabiki mmoja alisema: “Mike Dean refa wa mechi ya Arsenal na United? Yeah, hongera kwa watakaopewa penalti mbili na kushinda.”

Mwingine aliandika: “Mike Dean ameipa Man United penalti nyingi sana kuliko timu nyingine yoyote. Manchester United imekuwa wakipewa penalti katika kila mechi. Mustafi anatzamiwa kuanza. Hiyo ina maana tayari tumeshapigwa bao moja. Naamini timu itapambana kusawazisha!”

Shabiki wa tatu wa Arsenal alisema: “Huyu ni refa pekee anayewafanya mashabiki wa timu zote mbili kuwa na wasiwasi. Gwiji wa mchezo.”

Mechi ya mwisho ya Arsenal kucheza mwamuzi Dean akiwa uwanjani kuchezesha, alitoa penalti zote mbili na Watford ilishinda 3-2 dhidi ya kikosi hicho cha Mikel Arteta.

Alifanya kama hivyo kwenye mechi ya mwisho ya Man United ambapo Marcus Rashford na Joshua King wa Bournemouth wote walifunga kwa penalti katika mchezo uliopigwa Old Trafford ambapo wenyeji walishinda mabao 5-2.

Dean amechezesha mechi nne za Ligi Kuu England msimu huu na ametoa kadi 10 za njano na amewatoa nje kwa kadi nyekundu watu wawili wa West Brom mchezaji Kieran Gibbs na kocha Slaven Bilic katika mchezo dhidi ya Everton.

Kwenye mchezo huo, Dean atasaidiwa na Ian Hussin na Dan Robathan wakati mwamuzi wa akiba ni Anthony Taylor.

Peter Bankes atakuwa kwenye chumba cha VAR na atasaidiana na Neil Davies huko Stockley Park.

Hata hivyo, mashabiki wa Man United nao wameonyesha kutofurahishwa na uteuzi wa Dean, ambapo mmoja aliandika kwenye Twitter: “Hongera sana Arsenal, mtapata ushindi wenu wa kwanza wa Big Six kwa ugenini tangu Januari 2015.” Shabiki mwingine aliandika: “Faida kwa Arsenal.”