De Gea safii, Pogba huo sio mpango

Tuesday July 23 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND.HUO sio mpango nyie mjue. Juan Mata amewaambia David de Gea na Paul Pogba wapuuze uvumi wa kuhama na watulie Manchester United.

Mazungumzo ya kuongeza mkataba wa De Gea yanaenda vizuri kiasi cha kipa huyo kuthibitisha anabaki Old Trafford kwa ajili ya kupigania mataji huku akiomba apewe kitambaa cha unahodha, lakini mambo bado hayajawa mazuri kwa Pogba.

Pogba, kwa upande wake, ameshaeleza nia yake ya kutimka katika dirisha hili la uhamisho, huku Real Madrid na Juventus zikichuana kuwania saini yake.

Mata anaona kwamba masupastaa hao wawili ni muhimu sana kubaki OT na ndiyo turufu ya United katika kuanza zama mpya za mafanikio ya Mashetani Wekundu, huku akimtaja Pogba kuwa “ni mhamasishaji mzuri kwa kila mtu” na De Gea ni “kipa bora duniani”.

“Sote tunatambua kwamba Paul ni kiungo bora, na pia ni mtu poa sana, mwenye mawazo chanya, na mwenye ushawishi mzuri kwa kila mmoja.

“Nadhani ana furaha na anawaleta pamoja kila mtu, lakini siwezi kuwazungumzia watu wengine - najizungumzia mwenyewe.

Advertisement

“Kama mchezaji mwenzangu na pia rafiki tangu ningependa abaki kwasababu ni mchezaji wetu mzuri sana.”

Mata kisha akamsifu Mhispaniola mwenzake De Gea, ambaye ameripotiwa kuafiki dili mpya ya kubaki Man United na anakaribia kumwaga wino.

Aliongeza: “David ni kipa bora duniani na ni mmoja wa marafiki zangu wakubwa hivyo napenda abaki.

“Kiuweledi, litakuwa jambo kubwa kama atabaki kwa sababu atatupa pointi nyingi katika msimu unaokuja, hivyo nitafurahi sana akibaki.”

United katika mechi zake za kujiandaa na msimu ziarani Australia ilizifunga Perth Glory na Leeds na ikaichapa pia Inter Milan 1-0. Keshokutwa Alhamisi itaivaa Tottenham.

Watafungua msimu wa EPL dhidi ya Chelsea Agosti 11.

Advertisement