Dawa ya Ole ni hii hapa

Muktasari:

Katika kumaliza tatizo hilo, Solskjaer amepewa majina ya wachezaji ambao anapaswa kuyajumuisha kwenye kikosi chake kuifanya safu yake ya ushambuliaji kuwa na uwezo wa kupenya ngome yoyote ile ya mabeki wa timu pinzani.

MANCHESTER ,ENGLAND .OLE Gunnar Solskjaer ameambiwa wazi kikosi chake cha Manchester United msimu huu kina shida moja tu, kukosa mchezaji wa kuzisambaratisha ngome za timu pinzani.

Shida hiyo imeonekana kuigharimu Man United katika kupata mabao mengi kwenye mechi na hivyo kujikuta ikiishia kufunga bao moja tu kwenye mechi kibao jambo ambalo limekuwa likiigharimu.

Ukicheki rekodi za Man United haizidi mara tatu, ambapo ilicheza mechi na kupata ushindi wa kuanzia mabao mawili na kuendelea. Katika kumaliza tatizo hilo, Solskjaer amepewa majina ya wachezaji ambao anapaswa kuyajumuisha kwenye kikosi chake kuifanya safu yake ya ushambuliaji kuwa na uwezo wa kupenya ngome yoyote ile ya mabeki wa timu pinzani.

Mesut Ozil

Gwiji wa Man United, Paul Scholes ni shabiki mkubwa wa kiungo wa Kijerumani, Mesut Ozil na hivyo kumwambia Kocha Ole Gunnar Solskjaer kufanya mchakato wa kuinasa huduma ya staa huyo. Maisha ya Ozil huko Arsenal sio mazuri kabisa, Kocha Unai Emery amekuwa hamtendei haki kwa kumweka benchi licha ya kuwa kwenye kiwango bora kabisa. Scholes anaamini Ozil ndiye mchezaji ambaye Man United inamkosa.

Christian Eriksen

Kiungo Christian Eriksen amekuwa gumzo kwenye dirisha la usajili kwa muda mrefu. Mkataba wake huko Tottenham Hotspur unaelekea mwishoni jambo linalomfanya kuwa mchezaji huru itakapofika mwisho wa msimu, hivyo atakuwa huru kuondoka bure Juni mwakani. Lakini, suala la kupigwa bei linaweza kufanyika kwenye dirisha la Januari na Man United inaweza kuchangamkia huduma yake ikamnasa akafanye mambo.

James Maddi son

Kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Man United iliivamia Leicester City kunasa huduma ya Harry Maguire na sasa inafikiria kuvamia tena kwenye timu hiyo kunasa huduma ya kiungo fundi, James Maddison. Kwenye kikosi cha Leicester, Maddison anafanya vyema kwenye namba 10, eneo ambalo Man United inahitaji kuliboresha ili kukifanya kikosi kuwa na uwezo wa kupenya ngome za wapinzani.

Hakim Ziyech

Man United inaendelea na mchakamchaka wake wa kumfukuzia winga wa Ajax, Hakim Ziyech wakimhitaji akakipige kwenye kikosi chake. Ajax inasifika kwa kuwa kiwanda cha kuzaliwa wachezaji na ndani ya miezi michache iliyopita imeshuhudia mastaa wake Frenkie De Jong na Matthijs De Ligt wakiondoka kwenye timu hiyo na huenda Ziyech akaungana nao kuondoka kwenye kikosi.

Jadon Sancho

Mmoja wa makinda moto kwa sasa Borussia Dortmund na haiwezi kumwaachia kwa pesa kiduchu. Miamba hiyo imeripotiwa kuweka kipengele cha Pauni 100 milioni kwenye mkataba wake.