David Silva atoa mkono wa kwaheri Man City

Friday September 14 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND. Kiungo wa Manchester City, David Silva amefichua hana mpango wa kusaini mkataba mpya kwenye timu hiyo huku akibainisha mipango yake ya kwenda kumalizia soka lake kwenye kikosi cha Las Palmas.

Silva ni kipenzi cha mashabiki huko Etihad, akiwa ameichezea Man City mechi 349 kwa kipindi cha miaka minane aliyodumu kwenye timu hiyo.

Mkataba wake utafika tamati 2020 na baada ya hapo amesema hawezi kuendelea kubaki Man City.

Silva msimu uliopita mara kwa mara alikuwa akisafiri kurudi kwao Hispania kwenda kumwona mwanaye wa kiume, Mateo, ambaye alizaliwa wiki 15 kabla ya wakati, hivyo aliwekwa kwenye uangalizi mkubwa hospitalini kupambania uhai wake.

"Hapa Man City nataka kucheza kwa misimu mingine miwili tu, iliyobaki kwenye mkataba wangu," alisema Silva.

"Baada ya hapo, sifahamu. Itategemea na ninavyokuwa kimwili na kiakili. Nimekuwa nikisema siku zote nitapenda kuichezea Las Palmas, timu ya nyumbani. Lakini tusubiri kuona kitakachotokea kwa miaka hiyo miwili kutoka sasa."

Las Palmas ilishuka daraja kutoka kwenye La Liga msimu uliopita baada ya kushinda mechi tano tu kati ya 38 ilizocheza.