Data zinavyomaliza utata wa nani zaidi Emery, Solskjaer

Muktasari:

  • Tangu alipotua Man United kuchukua mikoba ya Mourinho, Desemba mwaka jana, Solskjaer hakuna kitu kingine kinachomhusu yeye zaidi ya kupewa sifa tu kutokana na kile alichokifanya kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

LONDON,ENGLAND. MASHABIKI wa Arsenal wanashangaa kwa nini kocha wao Unai Emery hasifiwi sana wakati rekodi zake kwenye mechi 19 za mwanzo klabuni hapo hazijatofautiana sana na za Ole Gunnar Solskjaer huko Manchester United.

Ni mjadala ulioibuka huko kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutazamwa kwa rekodi za makocha hao wawili katika mechi zao 19 za kwanza kwenye vikosi hivyo vya Arsenal na Man United.

Lakini, kuna shabiki mmoja amedai Emery alipata muda wa kuwa na kikosi kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya, wakati Solskjaer amekuja katikati ya msimu na timu ikiwa kwenye majanga baada ya kuboronga chini ya Jose Mourinho.

Tangu alipotua Man United kuchukua mikoba ya Mourinho, Desemba mwaka jana, Solskjaer hakuna kitu kingine kinachomhusu yeye zaidi ya kupewa sifa tu kutokana na kile alichokifanya kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

Kocha Emery kwenye mechi zake 19 za mwanzo klabuni Arsenal, ameshinda mara 13, ametoa sare nne na kupoteza mara mbili.

Kwa maana hiyo kwenye mechi hizo 19, kama ni pointi, Emery amevuna 43. Huku kikosi chake kikifunga mabao 41 na kuruhusu mabao 20 kwenye nyavu zao. Kwa mechi hizo 19, Emery alipaswa kuvuna pointi 57, lakini kwa 43 alizozipata hiyo ina maana amepoteza pointi 14.

Kwa upande wa Solskjaer kwenye mechi hizo 19, ameshinda 14, sare mbili na amepoteza mechi tatu. Kikosi hicho cha Man United chini yake kimefunga mabao 40 na kufungwa 17. Kwa maana hiyo, kikosi hicho cha Solskjaer kimevuna pointi 44, moja zaidi ya alizovuna Emery huko kwenye kikosi cha Arsenal katika mechi zake 19 za mwanzo.

Kwenye kipengele cha tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, Emery kikosi chake kina chanya ya 21, wakati Ole kikosi chake kina chanya ya 23. Kama ingekuwa kushinda mechi zote, basi Ole angepaswa kuvuna pointi 57, lakini kwa 44 alizopata hiyo ina maana chama lake la Old Trafford limepoteza pointi 13.

Mjadala huo wa mashabiki unaendelea huko kwenye mtandao wa Reddit, mashabiki wa Arsenal walikuwa wakiamini kocha wao Emery ana rekodi nzuri kwenye mechi zake 19 za kwanza kuliko za Solskjaer alizowaongoza Man United.

Mechi mbili alizopoteza Emery ni zile mbili za mwanzo wa msimu, aliponyukwa na Manchester United ya Pep Guardiola na Chelsea ya Maurizio Sarri. Mechi hizo zote mbili ni za Ligi Kuu England. Vichapo vitatu vya Ole Gunnar alikumbana navyo, dhidi ya Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kisha dhidi ya Arsenal Ligi Kuu England na Wolves kwenye robo fainali ya Kombe la FA.

Kuhusu Emery kutopewa sifa, shabiki mmoja aliandika: “Hii inatokana na sisi mashabiki wenyewe kwa sababu inashangaza na jinsi lawama zote anazoelekezewa Emery msimu huu.”

Lakini, shabiki mwingine alisema: “Huo ni mzaha. Hebu cheki kwa sasa tumekuwa hata na uhakika tunakwenda kukabiliana na timu za Top Six tukiwa na imani tutashinda ikiwa ni tofauti na miaka mingi iliyopita.”

Mwingine alikuja kusema Emery amekuwa na timu tangu kwenye maandalizi ya msimu kuanzia, lakini Ole amekuta timu ikiwa kwenye hali, lakini akifanya kweli kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Arsenal wao wapo kwenye Europa League huko. Huo ndio mjadala uliopo huko na mwingine alikuja kuhitimisha kwa kusema Solskjaer hana uzoefu kwenye ukocha kama aliokuwa nao Emery, hivyo anachokifanya huko Man United akiwa kocha wa muda hakina ubishi, kinahitaji kupewa pongezi.