Dante ngoma bado mbichi mjue

Muktasari:

“Dante akilipwa pesa yake anatakiwa arejee kwenye timu yake, lakini pesa iliyobaki nyingine atalipwa kidogo kidogo ndani ya miezi mitatu,” alisema.

SAKATA la beki Andrew Vicent ‘Dante’ na klabu yake ya Yanga limefikia mwisho baada ya pande zote mbili kuafikiana juzi Alhamisi jioni katika kikao cha Kamati ya Hadhi na Sheria za Wachezaji ya Shirikisho la Soka (TFF).

Katika kikao hicho kilichoanza saa 6 mchana hadi saa 9 alasiri, alikuwapo mchezaji husika pamoja na Mwanasheria wake, Alfred Mtawa na upande wa Yanga ukiongozwa na mwanasheria wao, Simon Patrick na walikubaliana Dante arejee kikosini, huku klabu hiyo ikipewa masharti mawili ya kutimiza.

Sharti la kwanza ni kulipa Sh30 milioni taslimu ndani ya siku saba, huku sharti hilo likiomnekana ni gumu, hata hivyo kamati iliamuru endapo itashindikana watakata kwenye pesa ya udhamini inayoingia kutoka Bodi ya Ligi.

Sharti la pili ni mchezaji husika kutotengwa ndani ya Yanga na badala yake kupewa muda wa kucheza kama ilivyokuwa awali kutokana na mchezaji huyo muda wote aliokuwa nyumbani akifanya mazoezi binafsi. Mjumbe mmoja wa kamati hiyo alilidokeza Mwanaspoti wameamuru mchezaji huyo arejee lakini wameweka masharti ambayo Yanga wanatakiwa wafuate pamoja na mchezaji husika.

“Kuna kiasi ambacho Yanga wameambiwa wampe Dante kama nusu na robo ya pesa anayodai, pesa hiyo inatakiwa itoke ndani ya siku saba, wasipofanya hivyo watakuwa wanakiuka maamuzi ya kamati, hivyo hatua ya kinidhamu itachukuliwa dhidi yao,” alisema.

Mjumbe huyo aliongeza mchezaji (Dante) kama akilipwa pesa hizo ndani ya siku saba anatakiwa ajiunge mara moja.

“Dante akilipwa pesa yake anatakiwa arejee kwenye timu yake, lakini pesa iliyobaki nyingine atalipwa kidogo kidogo ndani ya miezi mitatu,” alisema.

WANASHERIA WAFUNGUKA

Mwanaspoti halikuishia hapo kwani lilimtafuta mwanasheria wa Dante, Mtawa ambaye alisema kitu ambacho walikuwa wakikipigania ni mchezaji wao kupata stahiki zake na tayari kimefanikiwa.

“Sisi tulikuwa hatutaki kauli za mdomo bali za maandishi na tumefanikiwa katika hilo, kwani pesa atalipwa na nyingine zitatoka Bodi ya Ligi tumeambiwa,” alisema.

Mtawa aliongeza amefurahishwa na kamati hiyo kwa kuweka onyo la kuhakikisha mchezaji anacheza ili kuendelea kuwa katika kiwango chake.

“Wameonywa mchezaji akirudi aendelee kujisikia yupo nyumbani, apewe nafasi yake na hilo tunajua lipo vizuri kwa sababu mchezaji alikuwa anafanya mazoezi muda wote aliokuwa nje ya uwanja,” alisema.

Kwa upande wa Mwanasheria wa Yanga, Patrick alisema, “Dante ameambiwa arejee klabuni kama akishindwa kuja kwa wakati basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.”

Kesi hii imeunguruma takribani miezi mitatu huku Dante akiwa hajacheza mchezo wowote msimu huu.