Dante atoweka Yanga, Yondani kuiwahi Lipuli

Muktasari:

Yanga itacheza saa 10:00 jioni leo Julai 22, 2020 dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro huku ikielezwa kuwa kila mmoja ana sababu yake.


MABEKI wawili wa Yanga, Kelvin Yondani 'Cotton' na Andrew Vicent 'Dante' hawakusafiri na timu kuelekea Morogoro ambapo leo Jumatano Julai 22, 2020 wana kibarua cha kucheza na Mtibwa Sugar.

Mechi hiyo itachezwa saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku ikielezwa kuwa kila mmoja ana sababu yake.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael ameiambia Mwanaspoti Online kuwa hana taarifa kamili juu ya Dante kwani ni wiki nyingi zimepita hajamuona mazoezini na kwamba kuna mwendelezo wa utovu wa nidhamu kwa wachezaji wengi kukosa mazoezi bila kutoa taarifa kwake.

"Dante sijamuona kwa kipindi kirefu na kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa na mwendelezo wa kukosa mazoezi mara kwa mara, jambo ambalo nitaliweka katika ripoti yangu na kuona jinsi gani linaweza kufanyiwa kazi na uongozi kwani wao ndio jukumu lao," amesema.

"Kuhusu Yondani alinieleza kuuwa ana matatizo ambayo yanamalizika leo Jumatano, baada ya hapo nimemweleza anatakiwa kujiunga na timu ili kuwahi kucheza mechi ya Lipuli kwani ukiangalia wakati huu timu yetu inakosa wachezaji wengi muhimu ambao wana shida mbalimbali.

"Mechi yetu na Mtibwa kutakuwa na mabadiliko katika maeneo mengi kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji lakini hilo ndilo jukumu langu kahakikisha nawafundisha waliokuwepo ili Yanga iweze kuvuna pointi tatu bila kuangalia tunazungukwa na matatizo yapi," amesema Eymael.

Eyamel aliyechukua mikoba ya kukinoa kikosi hicho Desemba mwaka jana, imeiongoza Yanga katika mechi 25 za Ligi Kuu Bara na kabla ya kucheza na Mtibwa Sugar alikuwa ameshinda 11, amepoteza tatu na kutoka sare 11.

Kabla ya mechi hiyo na Mtibwa Sugar, Yanga imekusanya pointi 68 ikishika nafasi ya pili huku Azam ambayo pia inawania nafasi ya pili ikiwa na pointi 66, Azam wao watacheza kesho Jumatano na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex.