Dante akwepa rungu kiulaini

Muktasari:

  • Dante alipelekwa kamati ya nidhamu ya TFF kutokana na kitendo chake cha kutaka kumpiga kichwa mwamuzi wa kati wa mchezo kati ya Prisons na Yanga uliofanyika Mbeya.

MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu kufurahia baada ya beki wao, Andrew Vincent ‘Dante’ kukwepa rungu la Shirikisho la Soka nchini (TFF) wakati kikosi chao kikijiandaa kushuka uwanjani kesho Jumanne kuvaana na Mwadui katika mechi ya Ligi Kuu.

Dante alikuwa amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu aliofanya kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya Prisons, lakini kama zali tu jamaa amechomoka kuning’inizwa kwa kutokuwa na hatia.

Habari za kuaminika kutoka kwenye kikao cha kamati hiyo inaeleza Dante hajakutwa na hatia hiyo hivyo kunusurika kuanza mwaka na kifungo.

Dante juzi Jumamosi alipelekwa mbele ya kamati ya nidhamu akituhumiwa kumpiga mwamuzi wa mchezo huo dhidi ya Prisons uliopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya Desemba tatu na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Shtaka hilo la Dante awali lilitoka katika kamati ya saa 72 ambao walishindwa kulitolea uamuzi na kulipeleka kamati ya nidhamu.

Hata hivyo akiwa mbele ya kamati na nidhamu beki huyo alishindwa kutiwa hatiani kufuatia ushahidi kutojitosheleza na kuachiwa huru, ingawa alipewa onyo.

Akizungumza na Mwanaspoti Dante ambaye ni nahodha msaidizi wa Yanga, alisema ameambiwa hataweza kupewa adhabu kutokana na kamati kujiridhisha hakumpiga mwamuzi kama shtaka linavyosema.

Dante alisema kamati ilishangaa kuona shtaka lake limetoka Bodi ya Ligi (TPLB) huku ripoti ya mwamuzi ikiwa haijaonyesha lolote juu ya kilicholalamikiwa juu ya tukio husika.

“Nimeambiwa sina kosa katika shtaka husika, kamati imeshindwa kuona kama nilimpiga mwamuzi, hivyo nashukuru sasa presha imeshuka na kuendelea na kazi yangu,” alisema Dante.

Katika hatua nyingine Yanga leo Jumatatu inaendelea na mazoezi yake kujiandaa na mchezo wao wa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Mwadui, ikitaka kuilinda rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote, ikiwa timu pekee msimu huu.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 50 baada ya mechi 18, wakishinda 16 na sare mbili, huku ikijikusanyia mabao 35 na kufungwa 12, huku straika wao, Haritier Makambo akiwa mabao 11.