Dani Alves anavyowaburuza wenzake kwa kubeba mataji

Muktasari:

  • Kutokana na hilo, Alves aliyewahi kucheza Barcelona na Juventus anawaongoza mastaa kibao kwa kunyakua mataji mara nyingi ikiwamo hawa watano bora kabisa orodha inayowahusu mastaa wawili wa kutoka Afrika na Wabrazili wawili huko Mhispaniola akiwamo mmoja, fundi wa mpira, Andres Iniesta.

PARIS,UFARANSA.PARIS Saint-Germain wamebeba tena ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa. Lakini, jambo hilo limemfanya beki wa kulia, Mbrazili Dani Alves, anayecheza timu hiyo kuweka historia ya kuwa mchezaji aliyenyakua mataji mengi zaidi kuliko yeyote katika dunia ya mchezo huo.

Kutokana na hilo, Alves aliyewahi kucheza Barcelona na Juventus anawaongoza mastaa kibao kwa kunyakua mataji mara nyingi ikiwamo hawa watano bora kabisa orodha inayowahusu mastaa wawili wa kutoka Afrika na Wabrazili wawili huko Mhispaniola akiwamo mmoja, fundi wa mpira, Andres Iniesta.

5. Ibrahim Hassan -mataji 37

Gwiji wa Misri, Ibrahim Hassan amebeba jumla ya mataji 37 katika zama zake alizokuwa mchezaji kwenye klabu yake na timu ya taifa. Kwa muda mwingi wa soka lake, Hassan alicheza kwenye nchi yake ya Misri, huku akiicheza timu yake ya taifa mara 125 na kwenda kutamba katika kikosi cha Al Ahly katika zama mbili tofauti.

Staa huyo ameingia kwenye ile tano bora ya wachezaji waliobeba mataji mengi duniani kutokana na viwango vyao moto na bahati ya kunyakua mataji kwa nyakati zake alizokuwa akicheza.

4. Maxwell - mataji 37

Mchezaji wa Kibrazili, Maxwell kwa sasa amestaafu, lakini akiacha kumbukumbu za kuwa mchezaji aliyebeba mataji mengi sana katika maisha yake ya soka aliyokuwa akitamba huko Ulaya.

Beki huyo wa kushoto, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi msaidizi wa michezo kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain amebeba mataji 37 makubwa baada ya kupita kwenye vikosi matata kabisa, Ajax, Inter Milan, Barcelona na PSG, ambako kote alitamba na kubeba ubingwa wa michuano mbalimbali na hivyo kumfanya aingie kwenye orodha hii ya wakali waliojibebea mataji mengi kwenye soka la dunia.

3. Andres Iniesta -mataji 37

Bila shaka, Andres Iniesta kumbukumbu zake kwenye soka la ushindani anatambulika kama mmoja wa viungo bora kabisa waliowahi kutokea katika mchezo wa soka. Staa huyo alipokuwa kwenye kikosi cha Barccelona hakika alikuwa hakamatiki ndani ya uwanja na ndiko alikobeba mataji yake mengi pamoja na yale mengine aliyonyakua akiwa na timu ya taifa ya Hispania. Kwenye historia yake, Iniesta amebeba mataji 37 makubwa na hivyo kuwa mmoja wa wachezaji walionyakua mataji mengi duniani, huku moja ya mataji hayo ikiwamo Kombe la Dunia na ubingwa wa Ulaya huku Barcelona ikimpa mataji kibao ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka yake 16 aliyodumu kwenye timu hiyo.

2. Hossam Hassan -mataji 41

Kinara wa muda wote wa mabao wa Misri, Hossam Hassan aliweka rekodi hiyo baada ya kufunga mara 69 katika mechi 169 alizochezea timu yake ya taifa huku akiwa na rekodi tamu kabisa kwenye maisha yake ya soka kwa kubeba mataji 41. Staa huyo maisha yake ya soka alicheza kwenye klabu za Al Ahly na Al Ain na nyinginezo huku akiwa mchezaji namba mbili aliyebeba mataji mengi kwenye historia ya mchezaji wa sasa na sasa yupo huko kwenye Ligi Kuu Misri, anakotokea staa wa Liverpool, Mohamed Salah.

1. Dani Alves - mataji 42

Mwanasoka aliyebeba mataji mengi zaidi kwenye mchezo wa soka kwa sasa ni Dani Alves, ambaye kwa sasa amebeba mataji 42 katika historia yake katika mchezo huo. Mbrazili huyo amepita kwenye vikosi vya Sevilla, Barcelona, Juventus na sasa Paris Saint-Germain, ambako amekuwa na rekodi ya kujinyakulia tu mataji kama anavyotaka. Aliwahi kunyakua ubingwa wa Copa America akiwa na Brazil na hivyo kumfanya mchezaji huyo anayecheza beki ya kulia kuwa na rekodi ya kunyakua mataji mengi katika historia ya mchezo wa soka.