Dalali ataka taji

Monday April 16 2018

 

By OLIPA ASSA

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali amesema kinachoendelea ndani ya timu yake hiyo ni kutamanishwa ubingwa, lakini akadai safari bado ni ndefu na mapambano yanaendelea.

Amesema benchi la ufundi na wachezaji wanapaswa kuendelea kupambana hadi mwisho huku akikumbusha vitu vitatu vya kujihami navyo.

Kwanza, akasema Simba iwe makini inapocheza na timu zinazokaribia kushuka daraja na zinazotaka ubingwa kwa kuwa, zinakuwa moto kwelikweli.

“Simba kunanukia ubingwa hivyo wachezaji watambue kuwa kwa sasa ni kama kumposa mrembo anayetakiwa na kila mwanaume, ukizubaa inaweza kula kwako ukaishia kumwita shemeji.

“Ndivyo ilivyo kwa Simba, mwelekeo wa ubingwa usije ukawalevya na kusahau kuwa ndio wana kazi ngumu kuliko wanaowakimbiza, ambao hawana uhakika kama watawafikia au la, sasa vuta picha wao ndio wakafanikiwa kuchukua taji itakuwa ni aibu kubwa, lazima wawe makini,” alisema.

Alimshauri kocha Pierre Lechantre na Masoud Djuma, kuwaandaa wachezaji kisaikolojia ili wasivugwe na vitu vya kuwatoa mchezoni.

Wakati huo huo, Kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibaden alisema kwa wachezaji waliopo wa kikosi hicho, wana asilimia 99 za kuchukua ubingwa.

“Wakati huu ni kulinda umoja na mshikamano ili kufanikisha ubingwa, wasije wakadanganyika na sifa za mashabiki kuona wamemaliza, wana kazi nzito,” alisema.

Naye beki wa Salim Mbonde, alisema wakati walionao ni mgumu kwani wanahisi wamekamata roho za mashabiki ambao, wanadhani tayari ni mabingwa, hivyo ili wasije wakawasababishia matatizo wanalazimika kuwa waangalifu.