Dalali: Mnaosubiri Mo Dewji ajitoe Simba mtasubiri sana

Muktasari:

Katibu Mkuu wa tawi la Simba mkoa wa Arusha, Thabit Ustaadh amesema bonanza hilo ni kwa ajili ya kuwaunganisha wanachama wa Simba kutoka matawi mbalimbali ili kufahamiana pamoja na kuhamasisha mashabiki wengine kujiunga na matawi yaliyopo karibu nao.

SIKU chache baada ya kuwepo taarifa kwamba Mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji huenda akaachana na klabu hiyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali ameibuka na kutamka kuwa wanaosubiri mwekezaji wao kuachia ngazi watasubiri sana.
Ilielezwa kuwa, Mo Dewji alikusudia kuachia ngazi kwa madai ya kwamba hakuna maelewano mazuri na Mwenyekiti wa klabu, Swedy Mkwabi aliyedai anamhujumu na kushindwa kutekeleza baadhi ya mambo kwa wakati.
Dalali ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua tamasha la Matawi ya Simba yaliyoshirikisha michezo mbalimbali iliyofanyika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Dalali amesema ndani ya Simba hakuna mgogoro wowote na kinachoendelea kuzungumzwa mitandaoni ni uchonganishi.
"Kwa sasa tuko bize na usajili kuimarisha timu yetu na benchi zima la ufundi hivyo niwaambie wanachama wetu kuwa tuko vizuri na imara,  migogoro wanayosikia mitandaoni haina uhalisia ingekuwepo tungeisikia," anasema Dalali
Dalali amewapongeza tawi la Arusha kuunda matawi na kuwapa hamasa ya michezo ambapo amewaahidi kuwaunganisha baadhi ya wachezaji wazuri katika bonanza hilo na kamati ya usajili ili kufanya mazoezi ya majaribio.
Katibu Mkuu wa tawi la Simba mkoa wa Arusha, Thabit Ustaadh amesema bonanza hilo ni kwa ajili ya kuwaunganisha wanachama wa Simba kutoka matawi mbalimbali ili kufahamiana pamoja na kuhamasisha mashabiki wengine kujiunga na matawi yaliyopo karibu nao.
"Hili tamasha tutakuwa tunafanya kila mwaka Julai 7 kwa michezo mbalimbali mwaka huu timu 12 zimeshiriki michezo ya kuvuta kamba, kukimbiza kuku, soka na kukimbia kwa magunia" alisema Ustadh.