Dakika mbili za Ronaldo zilivyompeleka De Ligt Juventus

Muktasari:

Ushawishi wa Ronaldo katika mechi moja tu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ulibadili maisha ya beki huyo wa kati akizikacha klabu maarufu duniani Manchester United, Barcelona na Paris Saint Germain (PSG).

Turin, Italia. Haikuwa kazi nyepesi, lakini imewezekana. Nahodha wa Ajax Amsterdam, Matthijs De Ligt sasa ni mali ya mabingwa wa Ligi Kuu Italia Juventus.

Hakuna njia nyingine iliyotumika kumvuta De Ligt kwa ‘Kibibi Kizee’ hicho cha Turin zaidi ya kumtumia mshambuliaji wake nyota Cristiano Ronaldo.

Nahodha huyo wa Ureno alitumika kama chambo cha kumbeba kinda huyo mwenye miaka 19, aliyeng’ara katika mechi za Ligi ya Mabingwa UIaya msimu uliopita.

Ushawishi wa Ronaldo katika mechi moja tu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ulibadili maisha ya beki huyo wa kati akizikacha klabu maarufu duniani Manchester United, Barcelona na Paris Saint Germain (PSG).

Ilikuwa hivi. Ajax na Juventus zilicheza mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ronaldo alitumia takribani dakika mbili kumpa maneno matamu kinda huyo baada ya mechi kumalizika.

Licha ya kufungwa mabao 2-1, Ronaldo alitumia mwanya huo kumtaka De Ligt kuungana naye Juventus katika usajili wa majira ya kiangazi.

Vita ya De Ligt ilikuwa kubwa, lakini Ronaldo ameshinda na sasa De Ligt atavaa uzi wa Juventus msimu ujao.

Kama kuna mchezaji atakayechukiwa zaidi na Barcelona ni Ronaldo kwa kuzima ndoto zao za kumsajili De Ligt ambaye tayari alibakiza muda mfupi tu kutua Nou Camp.

De Ligt alimtanguliza mchezaji mwenzake wa Uholanzi, Frenkie de Jong Barcelona huku akiahidi kujiunga naye muda mfupi ujao kabla ya kubadili upepo.

“Napenda kucheza Barcelona lakini kabla ya sijafanya uamuzi ni lazima nijiridhishe kama nitakwenda kucheza kikosi cha kwanza, vinginevyo chaguo langu ni kucheza Ligi Kuu Hispania,”alikaririwa akisema De Ligt.

Kauli ya De Ligt ilipokewa vyema na mashabiki wa Barcelona wakiamini muda mfupi ujao watakuwa na beki kisiki namba tano mwenye kipaji cha aina yake.

Wakati Barcelona ikijiandaa kufanya sherehe ya kumpokea De Ligt, Ronaldo alibadili gia angani akitumia muda mfupi kumpeleka kwa kibibi kizee kwenda kuanza maisha mapya.

“Mara ya kwanza sikumuelewa anazungumza nini. Nilishituka, nilibaki kucheka, lakini sikumjibu chochote. Tukio hilo lilitokea muda mfupi sana baada ya kumalizika mchezo.

“Sikutarajia kama angenieleza maneno yale, kwanza ukizingatia timu yake ilikuwa imepoteza mchezo na katika hali ya kawaida unakuwa na mawazo mengi.

“Siku zote nilipenda kuwa mchezaji mkubwa kama Ronaldo, mimi na rafiki zangu wote tulikuwa na mawazo ya aina moja wakati tukicheza mpira kwenye bustani,”anafunguka De Ligt.

Libero huyo anasema ni shabiki mkubwa wa Ronaldo tangu akiwa nyota wa Man United na baadaye Real Madrid.

De Ligt anasema pamoja na ushawishi wa Ronaldo, amevutiwa na dau alilopata na alisifu kazi nzuri ya wakala wake Mino Raiola kufanikisha usajili wake.