Dakika 45 zimebaki kuamua Kagera Sugar, Mwadui kubaki ama kushuka

Muktasari:

Mwadui ndio walianza kutikisa nyavu za wapinzani wao kupitia mshambuliaji wao Salum Aiyee baadaye Geita walisawazisha kabla ya kwenda mapumziko kupitia Baraka Jerome.

MECHI ya mwisho ya mchujo kati ya Kagera Sugar na Pamba inasubiri kipindi cha pili kujua nani atacheza Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya dakika 45 za mwanzo kumalizika kwa suluhu, mechi hiyo inachezwa uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Wakati Kagera Sugar na Pamba wakitoka suluhu kipindi cha kwanza huko Shinyanga, Mwadui nayo imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita Gold dakika ya 45, mechi inachezwa uwanja wa Mwadui Complex.
Mwadui ndio walianza kutikisa nyavu za wapinzani wao kupitia mshambuliaji wao Salum Aiyee baadaye Geita walisawazisha kabla ya kwenda mapumziko kupitia Baraka Jerome.
Pamba inasaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu wakati Kagera Sugar inatetea nafasi hiyo ambapo mechi yao ya kwanza walitoka suluhu na dakika 90 ndizo zitakazoamua nani anapanda na atakayeshuka daraja.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza, Kagera Sugar ilikuwa inacheza kwa lengo la kuhitaji bao la mapema, iliweza kupata faulo na kona ambazo zilikuwa zinapigwa na David Luhende lakini hazikuzaa matunda.
Pamba wao walikuwa wanacheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza, huku eneo lao la kiungo likionekana kuzidiwa nguvu na Kagera Sugar.
Mbali na Pamba kucheza kwa kujilinda pia walikuwa wanaongoza kwa rafu ambapo Yusuph Dunia na Hassan Kabailo walilimwa kadi za njano kwa kucheza rafu.
Kagera Sugar ndio ilikuwa inafika langoni kwa wapinzani wao mara kwa mara lakini hata hivyo hawakuweza kuambulia kitu.