Dakika 180 zambeba Aussems

Muktasari:

Simba inavaana na UD Songo ikiwa na kumbukumbu ya kufika robo fainali ya michuano iliyopita kwa kukwamishwa na TP Mazembe ya DR Congo.

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema hana hofu yoyote katika mchezo wao wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji kwa vile anaziamini dakika 180 walizonazo zitawabeba na kuwabvuahs raundi ya kwanza ya michuano hiyo.
Aussems na jeshi lake likiwa mjini Beira, amesema anajua leo wana mchezo mgumu dhidi ya wenyeji wao pambano litakalochezwa kuanzia saa 10 jioni, lakini bado ana matumaini kama atashindwa kupata matokeo dakika 90 za kwanza bado ana 90 nyingine.
 “Tuna heshima kubwa kwa wapinzani wetu na tunajua utakuwa mchezo mgumu. Tuna michezo miwili, kesho (leo) na mwingine Dar na lengo ni kufuzu hatua inayofuata,” alinukuliwa Kocha Aussems juu ya mchezo huo wa leo.
Simba inavaana na UD Songo ikiwa na kumbukumbu ya kufika robo fainali ya michuano iliyopita kwa kukwamishwa na TP Mazembe ya DR Congo.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana, ila Simba ikiwa na kumbukumbu ya kung'olewa na  Têxtil do Punguè  mwaka 2007 katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 5-3 baada ya sare ya 1-1 ugenini na kulala nyumbani 4-2.