Dah! Samatta hatihati kuivaa Leicester City

Muktasari:

Kocha Dean Smith, ambaye alianzisha vikosi vinne mfululizo bila ya kuwa na straika, naye anahitaji fowadi wake huyo mpya mwenye umri wa miaka 27 awapo kwenye mchezo dhidi ya Foxes.

BIRMINGHAM, ENGLAND . ASTON Villa inasubiri kwa hamu straika wao mpya Mbwana Samatta apate kibali cha kazi ndani ya wiki hii ili wamtumie kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Ligi dhidi ya Leicester City Jumanne ijayo.

Samatta mapema wiki hii alikamilisha uhamisho wake wa Pauni 10.5 milioni kutoka Genk kwenda Villa Park, lakini staa huyo wa kimataifa wa Tanzania atahitaji kibali cha kazi kwanza kabla ya kuanza kuitumikia timu yake mpya.

Mashabiki wa Aston Villa na Watanzania wanasubiri kwa hamu kumwona ‘Champion Boy’ akifanya mambo yake huko kwenye kikosi hicho cha Ligi Kuu England.

Kocha Dean Smith, ambaye alianzisha vikosi vinne mfululizo bila ya kuwa na straika, naye anahitaji fowadi wake huyo mpya mwenye umri wa miaka 27 awapo kwenye mchezo dhidi ya Foxes.

“Tulihojiwa kuhusu mambo ya kibali cha kazi na tunaamini kitakamilika na tutakuwa naye mazoezini hadi mwishoni mwa wiki, jambo ambalo litamfurahisha kila mtu,” alisema Smith.

“Mechi yetu na Watford ilikuwa ya nne kucheza bila ya straika asili. Anwar El Ghazi, Jack (Grealish) na Trezeguet wamekuwa wakitumika. Indiana Vassilev naye pia amekuwa akitumika kwenye hilo.”

Aston Villa imekosa huduma ya straika wake namba moja tangu Wesley alipopata majeruhi ya goti yanayomweka nje kwa msimu wote. Kocha Smith alisema kwamba hajawahi kumtazama Samatta akicheza na kwamba, mtu aliyemfuatilia mchezaji huyo na kufanya asajiliwe Villa Park ni mkurugenzi wa michezo, Jesus Garcia Pitarch.

“Bado sijamwona ‘live’, lakini nilitazama video nane au tisa hivi za mechi ambazo alicheza,” alisema Smith.

“Suso ndiye mtu aliyemwona na skauti wengine tuliowatuma wakamtazame. Ni mfungaji mabao ni mwanamichezo wa kweli. Kama kuna aliyetazama Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu basi atakuwa ameona mabao yake, likiwamo lile la kichwa matata kabisa dhidi ya Liverpool. Nasubiri kwa hamu kufanya naye kazi.”

Kuhusu Samatta kucheza dhidi ya Leicester City kwenye Kombe la Ligi limekuwa suala la utata ambao, ulihitaji kufanyika ufafanuzi mkubwa kama staa huyo wa Tanzania atakubalika kucheza.

Sky Sports iliwahi kuripoti kwamba Samatta hataruhusiwa kucheza dhidi ya Leicester City, lakini atakubalika kucheza kama Villa itafika fainali.

Lakini, kanuni za EFL kuhusu Kombe la Ligi haziko wazi, jambo ambalo linaonekana kutoa nafasi kwa Samatta kucheza kwenye mechi hiyo ya marudiano kama atapata kibali cha kufanya kazi.

Imeelezwa hivi, kila kitu kitategemea kama EFL imeitambua nusu fainali hiyo kama mechi moja au mechi mbili. Kama zitahesabika kuwa ni mechi mbili, basi Samatta atacheza kwenye mechi hiyo ya pili.

Kama itahesabika kuwa ni mechi moja, sawa na inavyokuwa kwenye Kombe la FA inapokuwa na marudio – Samatta hataruhuwiwa kucheza kwa sababu usajili wake umefanywa wakati mchezo wa kwanza ulishachezwa.

Kumekuwa na maelezo kwamba, kwa mujibu wa Twitter, Oumar Niasse aliichezea Hull City kwenye mechi ya pili aliposajiliwa baada ya mechi ya kwanza kumalizika. Kanuni hazipo wazi, lakini kwa hali ilivyo kwa sasa, Samatta atakuwa na nafasi kubwa ya kuwakabili Leicester City labda kama tu EFL wataamua vinginevyo. Mechi ya kwanza iliyopigwa King Power timu hizo zilitoka 1-1.