Dah! Msuva awavimbia Mane, Mahrez

Muktasari:

  • Lakini Msuva mwenye mabao 10 kwenye Ligi ya Morocco ‘Batola Pro’, alisema kila kitu huwa ni kujipanga na hakuna kinashindikana kwenye kundi hilo.

MSHAMBULIAJI wa Difaa El Jadida, Saimon Msuva amesema kinachoweza kuwabeba Taifa Stars katika fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri ni maandalizi kabambe na uzoefu wa kocha wao, Emmanuel Amunike.

Taifa Stars imepangwa Kundi C katika fainali hizo ambazo watashiriki kwa mara ya pili pamoja na Senegal, Algeria na Kenya.

Senegal inayoongoza Afrika katika viwango ubora wa soka vya FIFA ina wakali kibao kama Sadio Mane (Liverpool), Kalidou Koulibaly (Napoli), Cheikhou Kouyate wa West Ham, Idrisa Gueye (Everton), Biram Mame Diouf aliyekipiga Man U, Moussa Sow, Diafra Sakho na Armand Traore aliyewahi kukipiga Arsenal wakati Algeria ina nyota kama Riyad Mahrez wa Man City, Islam Slimani (Fenerbahce), Sofiane Feghouli (Galatasaray) na Yacine Brahimi wa FC Porto ya Ureno.

Lakini Msuva mwenye mabao 10 kwenye Ligi ya Morocco ‘Batola Pro’, alisema kila kitu huwa ni kujipanga na hakuna kinashindikana kwenye kundi hilo.

“Maandalizi mazuri yanaweza kutubeba, binafsi nilitegemea kupangwa dhidi ya mataifa ya Afrika Magharibi. Nadhani hili niliwahi kuliongelea. Mpira umebadilika, wasidhani kama wanaweza kutunyanyasa kama kipindi cha nyuma.

“Wanaweza wasiamini kitakachotokea. Kumdharau mshindani ni kitu kibaya. Sisi kutazamwa kama taifa dogo inaweza kuwa fimbo kwao ya kuwaadhibu,” alisema Msuva.

Msuva alisema mbali na maandalizi kingine kinachoweza kuwabeba ni uzoefu wa kocha wao, Amunike ambaye aliwahi kulibeba taji hilo akiwa mchezaji wa taifa lake la Nigeria.

“Ameshinda hilo kombe hivyo naamini ataendelea kutupa vitu ambavyo vitatusaidia kama wachezaji kulipigania taifa letu,” alisema Msuva.

Amunike ambaye alicheza Kombe la Dunia 1994, Marekani alikuwa sehemu ya kikosi cha Nigeria ambacho kilitwaa kombe katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa mwaka huo, Tunisia.