Dabi za kibabe FDL

PAZIA la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) litafunguliwa rasmi leo ammbapo jumla ya timu 20 zitaanza kusaka nafasi mbili za kupanda Ligi Kuu moja kwa moja huku nyingine zikipambana kuhakikisha angalau zinacheza mechi za mchujo za kuwania kupanda.

Ligi hiyo itakuwa na makundi mawili ambapo kundi A litakuwa na timu 10 ambazo ni African Lyon, African Sports, Gipco, Ndanda, Njombe Mji, Mbeya Kwanza, Mawenzi Market, Boma, Lipuli na Majimaji wakati kundi B litakuwa na timu za Geita Gold, Pamba, AFC, Transit Camp, Mbao, Alliance, Rhino Rangers, Singida United, Fountain Gate Academy na Kitayosce FC.

Mara nyingi kutokana na kiu na hamu ya timu kupanda Ligi Kuu, mechi za FDL huwa na ushindani mkubwa kuanzia mwanzoni hadi pale msimu unapokuwa katika dakika za lala salama.

Hata hivyo kuna mechi ambazo huwa na msisimko na ushindani mkubwa zaidi ya nyingine pengine kutokana na ukaribu wa timu husika na historia ya mechi zao za nyuma lakini sababu nyingine za hapa na pale.

Makala hii inakuletea orodha ya mechi ambazo hapana shaka zitakuwa na ushindani mkubwa na zinaweza kufuatiliwa kwa ukaribu katika Ligi Kuu msimu huu.

Fountain Gate vs Alliance

Msimu huu timu hizo zitakutana katika mechi ya kwanza ambayo Fountain Gate itakuwa Uwanja wa nyumbani wa Jamhuri,leo.

Kitendo cha timu hizo zote kuwa vituo vya soka, kinafanya wengi watamani kuona nani atatamba baina yao ukizingatia vituo vinavyozimiliki pia zina shule za elimu ya kawaida.

Dabi za Mwanza

Msimu huu, jiji la Mwanza halina timu katika Ligi Kuu lakini sasa wakazi wake watashuhudia uhondo katika FDL ambayo ina timu tatu kutoka mkoa huo.

Ni wazi mechi zitakazokutanisha timu za mkoa huo zitakuwa na ushindani mkali na miongoni mwa hizo ni ile ya Mbao ambayo ni timu iliyoanzishwa miaka ya hivi karibuni na timu kongwe ya Pamba.

Lakini pia kutakuwa na mechi baina ya Pamba na Alliance na mechi zingine mbili zitakuwa baina ya Alliance na Mbao.

Kitayosce vs Rhino Rangers

Baada ya kuwakilishwa na Rhino Rangers kwa muda mrefu katika FDL, safari hii Mkoa wa Tabora utakuwa na timu nyingine ambayo nyingine itakuwa ni Kitayosce.

Mechi baina ya timu hizo mbili inategemewa kuwa na upinzani wa hali ya juu kwani mbali na kila timu kusaka alama tatu, hapana shaka kila upande utataka kudhihirisha kuwa ni Mfalme wa Tabora.

Dabi za Nyanda za Juu Kusini

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iankimbizana na ile ya Magharibi kwa kuwa na idadi kubwa ya timu zinazoshiriki FDL msimu huu ambapo ina jumla ya timu sita ambazo ni Majimaji, Njombe Mji, Lipuli, Gipco, Boma na Mbeya Kwanza.

Timu hizo zote mbali ya kuwa na uzoefu na FDL, mechi baina yao wenyewe kwa wenyewe zinatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na nyingi kuwahi kukutana mara nyingi katika ligi hiyo ama Ligi Kuu hivyo zinafahamiana vyema.

Dabi ya Vidonde Katika kundi B kuna timu tatu ambazo zimeshuka daraja msimu uliopita na zitacheza FDL ambazo ni Singida United, Mbao na Alliance wakatika katika Kundi A kuna timu tatu ambazo ni Lipuli, Ndanda na Majimaji.

Timu hizi mbali ya kiu ya kurejea katika Ligi Kuu, kila moja nji wazi kwamba haiko tayari kuporomoka zaidi na kuangukia katika Ligi Daraja la Pili (SDL).

Siri pekee ya kufanikiwa ni kila moja kuhakikisha inapata ushindi dhidi ya mwenzake jambo ambalo ni wazi kwamba litakoleza ushindani pindi zitakapokutana.