DP Ruto, Sonko wamwaga noti kwa Harambee Stars

Muktasari:

Mara ya mwisho Stars kufuzu ilikuwa ni mwaka 2004, chini ya ukufunzi wa Jacob ‘Ghost’ Mulee. Bao lililoipeleka Stars Tunisia likiwekwa kimiani na Deniss Oliech (2003), walipoifunga Cape Verde 1-0, ugani Kasarani.

Nairobi, Kenya. Wachezaji wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ watakoga minoti kutokana na ahadi ya Naibu wa Rais, Dk. William Ruto ya Sh 50milioni pamoja na ile ya Sh 3milioni kutoka kwa Gavana wa Jiji la Nairobi, Mike Sonko baada ya kuichapa Ethiopia kwa mabao 3-0.

DP Ruto alifika uwanjani hapo majira ya saa tisa alasiri, chini ya ulinzi mkali alishangiliwa na mashabiki hao, hasa baada ya kuahidi kuipatia Stars, Sh50 milioni endapo ingeifunga Ethiopia, kazi iliyofanywa na Eric Johanna, Michael Olunga na Victor Wanyama na kuipa Stars, ushindi wa 3-0.

Gavana wa Jiji la Nairobi, Sonko alitoa kitita cha Sh3 milioni kwa wachezaji Harambee Stars kwa ushindi huo unaotoa mwanga kwa Kenya kufuzu kwa fainali ya Afcon mwakani.

 Mchezo huo ulishudiwa na mashabiki 55,000 akiwamo Mwanaharakati, Mwanasiasa na Mwanamuziki wa Uganda, Robert Ssentamu ‘Bobi Wine’.

Katika mchezo huo Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ilitoa nafasi kwa mashabiki kuingia bure jambo lililotoa nafasi kwa mashabiki 55,000 kuujaza uwanja Moi Kasarani.

Endapo Stars, itafanikiwa kwenda Cameroon mwakani, itakuwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo baada ya miaka 14. Harambee Stars, sasa inaongoza kundi F, ikiwa na alama saba, ambapo mechi inayofuata itakuwa dhidi ya Ghana ugenini.