DJ Arafat amefariki dunia kwa ajali ya pikipiki

Muktasari:

Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo, Maurice Bandaman alisema kuwa pikipiki yake iligongana uso kwa uso na gari lililokuwa likiendeshwa na mwandishi wa habari wa Radio ya Taifa ya Ivory Coast.

Abidjan, Ivory Coast. Mwanamuziki maarufu wa mitindo ya Coupé-Décalé nchini Ivory Coast, Houon Ange Didier ‘DJ Arafat’ (33), amefariki dunia kwa ajali ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongwa na gari.

Tovuti ya CNN imeeleza kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia jana Jumatatu Agosti 12, 2019 ambapo nyota huyo alikuwa na marafiki zake wakielekea Abidjan, mji mkuu wa Ivory Coast.

Kwa mujibu wa Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo, Maurice Bandaman alisema pikipiki yake iligongana uso kwa uso na gari lililokuwa likiendeshwa na mwandishi wa habari wa Radio ya Taifa ya Ivory Coast.

CNN wameweka picha zikimuonyesha DJ Arafat akiwa amelala barabarani akiwa amepoteza fahamu ambapo aliwahishwa haraka hospitalini kutibiwa kabla ya kufariki dunia jana Jumatatu Agosti 12, 2019 saa 2:10 asubuhi.

Wakati wa uhai wake, DJ Arafat anayetumia miondoko ya kufoka foka aliwahi kutamba na nyimbo kadhaa na kuimba na wasanii wakubwa akiwamo J. Martins.

“Niko hospitalini muda huu alipokuwa amelazwa DJ Arafat na nathibitisha kuwa amefariki dunia,” Bandaman anakaririwa na Jeune Afrique.

Wimbo wa mwisho alioutoa ni ‘Moto moto’ ambao hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 4.4 kwenye YouTube ndani ya miezi mitatu.