DILUNGA : Mchana nyavu aliye na ndoto kibao kisoka

Muktasari:

  • Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Dilunga, ambaye ameeleza mikakati yake na ndoto ambazo anataka kuzifikia.

UKIANGALIA katika msimamo wa wafungaji kwenye Ligi Kuu Bara utaona jina la Herieter Makambo likiwa juu kabisa na mabao yake 11 kisha linafuata la Said Dilunga, ambaye ana mabao 10 hivyo kukifanya kinyang’anyiro cha kuwania Kiatu cha Dhahabu kikiwa kwenye changamoto kubwa.

Licha ya Makambo jina lake kuimbwa sana kweye soka la Bongo kwa sasa, lakini amekuwa na kazi kubwa mbele ya Dilunga, ambaye huwa hana mbwembwe nyingi na amekuwa akipasia nyavuni kimya kimya bila kelele.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Dilunga, ambaye ameeleza mikakati yake na ndoto ambazo anataka kuzifikia.

AMETOKA WAPI

Said kama ilivyo kwa wanasoka wengine nchini, alianza kucheza soka la mitaani na anafahamika sana pale Magomeni akiwa na chama lake la mtaani la Mesina. Baada ya kukipiga sana mchangani, Said alianza kujijenga na kutua klabu ya Mkungunya iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza Wilaya ya Ilala.

Mwaka 2009 alijiunga na Toto African ambako aliliamsha dude kinoma na kumaliza kwenye nafasi ya tatu ya wafungaji. Hakudumu sana kwenye kikosi hicho na mwaka uliofuata akatimkia zake Kagera Sugar na nyota yake iling’ara zaidi alipojisogeza Ruvu Shooting mwaka 2012.

“Nakumbuka nilivyokuwa Toto African msimu wangu wa kwanza tu nilikuwa katika orodha ya wafungaji bora msimu huo, lilikuwa jambo la furaha sana kwa sababu nilikuwa mgeni na Ligi,”.

KIPAJI CHAMPA GWANDA

Baada ya kung’ara akiwa Toto na Kagera Sugar, Ruvu Shooting walimpa ofa na akakubali kujiunga nao, lakini alipotua tu akapata zali la kuingizwa kwenye mfumo wa ajira ndani ya taasisi hiyo.

“Nakumbuka natoka Kagera nilikuwa na mabao nane, nilikuwa vizuri na ndoto nyingi za kucheza soka nje, lakini nilisaini Shooting na nikiwa na wiki mbili zikaja nafasi za kwenda kozi na ndipo nikaambiwa napaswa kwenda. Nilipomaliza mafunzo hayo fasta tu nikapewa gwanda,” anasema Said na kuongeza” Sikuwa na jinsi ilibidi nikubali tu kujiunga na Jeshi baada ya kuamini kwamba, alipangiwa na Mungu kuwa kwenye upande huo.

“Kabla sijajiunga na Shooting nilikuwa na mpango wa kwenda Ugiriki, lakini yule ambaye alikuwa ananifanyia mpango mimi na Boban alikamatwa baada ya kuzidisha muda wa kuishi kule, hivyo nikarudisha matukio ya nyuma nilipokwenda kufanya majaribio Oman na kufaulu, lakini sikusajiliwa kwa sababu dirisha lilifungwa”.

VIPI KUHUSU HASSAN DILUNGA

Mashabiki wengi wamekuwa wakijiuliza kama kuna undugu kati ya Hassan Dilunga na Said Dilunga, lakini hapa mwenyewe anaweka mambo hadharani.

“Ukoo wa Dilunga ni mpana sana na unatokea huku Uzaramuni hivyo, kiukoo ni ndugu kwa sababu wote tunatokea sehemu moja, lakini undugu wa karibu sio sana,” .

Anasema licha ya kuwa wote waliichezea Ruvu Shooting na walikuwa wakishirikiana katika kila jambo huku wakichukuliana kama ndugu.

“Baba yangu alicheza Simba, Hassan ninachojua ni kuwa tumefanana majina ya ukoo kwa sababu ni wazaramo, lakini tulipokuwa wote Shooting tulikuwa tunachukuliana kama ndugu,”.

ATAKA REKODI SHOOTING

Straika Abdulrahman Mussa aliandika rekodi ya kipekee katika kikosi cha Ruvu Shooting baada ya kufunga magoli 14 na kuchukua kiatu cha dhahabu.

Hata hivyo, Dilunga anafichua kuwa akili yake kwa sasa ni kuivunja rekodi iliyowekwa na Mussa ili atengeneze mpya kabisa ambayo itadumu kwa miaka kadhaa.

“Ndoto zangu zinaniambia kwamba natakiwa nifunge zaidi ya mabao 14, siwazii sana ufungaji bora lakini kama ikitokea sawa tu ila malengo ni kutengeneza rekodi yangu hapa. Sitaacha kabisa kufunga hata ikitokea nimefikisha idadi hiyo kwani, rekodi itazidi kusogea juu zaidi na atakayetaka kuivunja hapa itamchukua muda,” anasema.

KWANI MAKAMBO VIPI

Kasi ya Makambo, raia wa DR Congo katika kufunga kila shabiki na mpenzi wa soka nchini anaifahamu vyema kabisa, lakini wakati huo huo wazawa wamekuwa wakitupia zaidi kukimbizana na Mkongomani huyo.

Dilunga alikiri Makambo ni mchezaji mzuri na anajua kufunga pindi anapokuwa karibu na goli, lakini hapendi kuona tuzo hiyo ikienda kwa mchezaji wa kigeni.

“Ukimuona mshambuliaji ana uwezo wa kufunga magoli mawili katika mechi moja inabidi aogopwe sana, kiukweli Makambo analijua goli na anajua kusumbua mabeki ndio sababu anafunga, lakini safari hii tuzo ichukuliwe na mzawa,” alisema.

HAVUI GWANDA NG’O

Kama kulikuwa na timu inamtolea udenda straika huyo basi isahaue kabisa kwani, hana mpango wa kuvua gwanda.

“Nivue gwanda? Hapana siwezi kaka kwa sababu hapa unaponiona hata kama ikitokea imekuja kozi nitaacha soka na kwenda kwenye mafunzo, hii ndio kazi yangu na ninaipenda, kama magoli nitafunga ila kozi ni muhimu zaidi,” anasisitiza Said ambaye ni baba wa watoto wawili, Muzdalifa (9) na Jamali (5) kwa mkewe kipenzi Amina Khamis.