DELE ALLI AKATALIWA DILI LA STAA BALE

MADRID, HISPANIA. HABARI ndo hiyo. Real Madrid imeripotiwa kukataa ofa ya Tottenham Hotspur ya kumjumuisha Dele Alli kwenye mpango wao wa kumsajili winga matata, Gareth Bale.

Wakala wa winga huyo alifichua kwamba mteja wake anataka kurudi kwenye klabu yake hiyo ya zamani ili kukipiga katika Ligi Kuu England na mazungumzo yanaendelea ili kukamilisha dili hilo katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Los Blancos wao wapo tayari kuachana na Bale ili kuondokana na mshahara mkubwa wanaomlipa huku ikifahamika wazi kwamba kocha Zinedine Zidane hana mpango wa kutumia kwenye kikosi chake kwa msimu huu.

Hata hivyo, mishahara imeonekana kuwa tatizo huko Spurs na hilo linawafanya kutaka kumjumuisha Dele Alli kwenye dili hilo ili kupunguza gharama za matumizi ya pesa. Kwa mujibu wa The Express, Real Madrid haina mpango na Dele Alli, licha ya kwamba wana dhamira kubwa ya kumuuza Bale. Dili la kumnasa Bale litakuwa na mkopo wa msimu mmoja, licha ya kwamba Real Madrid inahitaji Pauni 18 milioni kwa timu ambayo itakuwa tayari kumchukua mchezaji huyo na kumlipa mshahara wake wote Pauni 600 kwa wiki.