Courtois amkingia kifua Hazard

MADRID, HISPANIA. GOLIKIPA wa Real Madrid, Thibaut Courtois amesisitiza staa mwenzake wa Real Madrid, Eden Hazard atakaa sawa na kuonesha kiwango kikubwa ndani ya timu hiyo baada ya kupata majeraha tokea ajiunge na miamba hiyo katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2019 akitokea Chelsea.

Hazard alikuwa anatazamiwa kuziba pengo la Cristiano Ronaldo baada ya kusajiliwa kwake kwa dau la Pauni 150 milioni lakini ameshindwa kufanikisha hilo kwa kuwa amekumbana na majeraha ambayo yanamfanya kuwa nje kwa muda mrefu na hata mwili kuzidi uzito.

Lakini mchezaji mwenzake wa Madrid na timu ya Taifa ya Ubelgiji Courtois ambaye pia hakuanza vizuri wakati anajiunga na miamba hiyo amesema mchezaji huyo atakaa sawa na kuonesha kiwango kikubwa.

“Sina wasiwasi kuhusu yeye, nina uhakika kuwa ataonesha kiwango kikubwa, nafahamu kuwa anatamani kuonesha ubora wake na nina matumaini atathibitisha hilo, kwa sababu kabla ya kupata majeraha alicheza mechi nyingi ambazo alionekana kucheza vizuri, lakini anaokana kuwa na bahati mbaya iliyopelekea kuwa nje,”alisema.

Courtois aliongeza Hazard tayari ameanza kufanya mazoezi na anaamini hatachukua muda mrefu kurudi kuonesha kiwango ambacho kitawafurahisha mashabiki wengi wa Real Madrid.

Hazard hajacheza mchezo wowote akiwa na timu hiyo kutokana na maumivu ya misuli aliyopata mara ya kwanza ambapo alipona lakini amekumbana na majeraha mengine ya kifundo cha mguu ambayo yameanza kupona.

Winga huyo ambaye alihudumu amecheza mechi 22 katika mechi 51 ambazo angeweza kucheza ikiwa asingepata majeraha ambayo yameonekana kumkera sana hadi yeye mwenywe.