Corona yatibua mipango ya Prisons

Muktasari:

"Mfano ligi ikianza Juni na ikatokea wapo wachezaji ambao mikataba yao itakuwa imeisha basi watamalizia na tutakuwa tunawapa mshahara, hiyo ndio itakayokuwa gharama kubwa kwetu kwani bajeti itakuwa imeongezeka,"

KATIBU Mkuu wa Tanzania Prisons, Ajabu Kifukwe amesema wanazitazama changamoto mbalimbali ligi itakapoanza kama gharama za wachezaji ambao mikataba yao ipo ukingoni.
Amesema endapo ligi ikianza ndani ya siku 30 basi kuhusu gharama halitawasumbua nje na hapo wanaona changamoto kubwa ya namna ya kuanza kukaa na wachezaji upya.
Amesema kwa kuwa ugonjwa wa corona haukupiga hodi,  basi wanajiandaa kukabiliana na kila changamoto itakayokuwa mbele yao ili mladi tu msimu uishe salama.
"Mfano ligi ikianza Juni na ikatokea wapo wachezaji ambao mikataba yao itakuwa imeisha basi watamalizia na tutakuwa tunawapa mshahara, hiyo ndio itakayokuwa gharama kubwa kwetu kwani bajeti itakuwa imeongezeka,"
"Kwa sababu hata wao wanajua kwamba ni janga la dunia, wameruhusiwa kwenda nyumbani ili kulinda afya zao bila shaka naamini watakuwa waelewa kwani hata wakikomaa kuondoka hata huko hawatacheza watasubiri ligi iishe," amesema.
Jambo analoona nafuu ndani ya kikosi chao ni kwamba sio wachezaji wengi ambao mikataba yao ipo mwishoni,  hivyo kama kuondoka watakuwa wachache.
"Wachezaji wengi ni askari, raia wachache ndio mikataba yao itaishi Juni, ila tupo tayari kukabiliana na hilo na kila kitu kitakwenda sawa"amesema.