Corona yamuua baba yake Totti

ROME, ITALIA. BABA mzazi wa staa wa soka, Francesco Totti, Enzo amefariki dunia kwa virusi vya corona akiwa na umri wa miaka 76.

Gwiji huyo wa Italia, Enzo, alifariki katika Hospitali ya Lazzaro Spallanzani iliyopo Rome, alikokuwa amelazwa Jumatatu iliyopita.

Enzo ameacha mke Fiorella na watoto Riccardo na Francesco.

Klabu ya AS Roma ilionyesha dhahiri kuguswa na kifo hicho ambapo ilikitangaza kupitia mitandao ya kijamii.

Kwenye Twitter ya klabu hiyo waliandika ujumbe uliosomeka: “Kwaheri Enzo. Pole zetu ni kwa Fiorella, Francesco, Riccardo na familia nzima kwa ujumla.”

Enzo alitajwa kwenye orodha ya watu waliokuwa kwenye hatari ya kushambuliwa na virusi hivyo baada ya kupatwa na shambulizi la moyo miaka michache iliyopita.

Katika kipindi cha miaka 25 ya mwanaye aliyokuwa akiichezea AS Roma, Enzo alikuwa akisafiri kwenda kwenye mechi za timu hiyo kila mahali.

Na alikuwa akihudhuria pia kwenye mazoezi na kuwaletea wachezaji pizza.

Ripoti kutoka Italia zinadai Enzo katika kipindi cha mwishomwisho cha uhai wake alijitolea zaidi kuwa karibu na wajukuu zake Cristian, Chanel na Isabel. Mashabiki walitumia kurasa za Twitter kumpa pole Francesco Totti