Corona yamshusha presha baba Msuva

Muktasari:

Msuva anachezea Difaa El Jadida ya Morocco aliyojiunga nayo mwaka 2017 akitokea Yanga ambayo ilimsajili mwaka 2011 kutoka Moro United.

BABA mzazi wa mchezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars Simon Msuva, Happygod Msuva amesema wanafarijika kuona makali ya virusi vya Corona yanapungua.

Msuva kwa sasa anakipiga katika timu ya Al Jadida inayoshiriki ligi Kuu nchini Morocco.

Akizungumza na Mwanaspoti leo, baba wa Msuva anasema, hata yeye kama mzazi anapata imani juu ya mwanae huko aliko kwa kuwa yuko mbali nae na hasa ikizingatia aliko mwanae maambukizi yalikuwa makubwa.

"Mwanangu huko Morocco walikuwa hawatoki hata ndani wakitaka kitu wanaagiza, basi ilikuwa inanitia sana hofu kama mzazi ila sasa hivi naona kuna nafuu hata tukiongea nae kwenye simu,"

Anasema hata katika vyombo vya habari katika nchi za nje inaonekana hali imepungua makali tofauti na siku za nyuma.

Aidha Mzee Happygod anasema, alitamani mwanae arejee nchini lakini ikawa ngumu kutokana na mazingira magumu ya usafiri kutokana na nchi nyingi kufunga mipaka na kuweka zuio la watu kutoka nje  

"Tunashukuru sana Mungu huko aliko mwanangu yuko salama ni faraja kwetu kama wazazi kwa kuwa ni lazima mimi kama mzazi niwe na hofu,"

Msuva alianza kucheza soka mwaka 2004/05 katika Academ ya Pangolin iliyokuwa ikifanya mazoezi yake Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam,  chini ya Kocha Boniface Mkwasa aliyekuwa akisaidiana na Evarist Katomondo.

Mnamo mwaka 2007/08 akajiunga na timu ya Chuo Kikuu iliyokuwa chini ya Mohamed Msemo, na baada ya hapo akashiriki timu ya Copa CocaCola mwaka 2009.

Mwaka 2010 alijiunga na timu ya Azam B na kushiriki michuano ya Uhai 2011 na kuibuka mfungaji bora katika mashindano hayo, na ndipo klabu ya Moro ikamnasa katika usajili wa dirisha dogo na kubahatika kucheza raundi ya pili na kutua Yanga na baadaye  Jadida.

Mbali na kandanda Msuva pia aliwahi kuwa mnenguaji katika kituo cha Nyumba ya Vipaji (THT) kilichopo jijini.