Corona yaibua mzozo mpya mastaa England kukatwa mishahara

Muktasari:

Wakati watumishi wengine wa klabu hizo wakiwamo walinzi wa uwanjani (stewards) wakikatwa asilimia 20 ya mishahara yao na kuingia katika mpango wa kuwezeshwa na serikali, mastaa wakubwa wa EPL wanaendelea kuvuta mamilioni kila wiki, na wameshauriwa na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kutokubali kukatwa mishahara yao.

LONDON,ENGLAND . HUKO Barcelona wachezaji wamekubali kukatwa asilimia 70 ya mishahara yao wakati wa janga la corona ili ichangie wahudumu wengine wa klabu hiyo walipwe asilimia 100 ya mishahara yao.

Kule Juventus wachezaji na kocha Maurizio Sarri wamekubali wasilipwe chochote kwa miezi minne katika mapambano hayo dhidi ya corona Italia, ambako vifo kutokana na ugonjwa huo vimeshazidi 13,155. Hispania inafuatia ikiwa na vifo 7,340.

Wachezaji wa klabu za Ujerumani za Bayern Munich na Borussia Dortmund pia wamekubali kukatwa mishahara.

Ishu sasa iko England ambako vifo vya corona vimefikia 2,352. Wanasiasa, wachezaji wa zamani na mashabiki wa soka wamezikosoa klabu za Ligi Kuu ya England kwa kushindwa kupunguza mishahara ya wachezaji wao ambao kiuhalisia wana utajiri wa mamilioni ya pesa na badala yake kuacha watumishi wengine wa klabu hizo wakikatwa mishahara, na hivyo kuingia katika mpango wa serikali wa kuwawezesha wenye vipato vidogo.

Wakati watumishi wengine wa klabu hizo wakiwamo walinzi wa uwanjani (stewards) wakikatwa asilimia 20 ya mishahara yao na kuingia katika mpango wa kuwezeshwa na serikali, mastaa wakubwa wa EPL wanaendelea kuvuta mamilioni kila wiki, na wameshauriwa na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kutokubali kukatwa mishahara yao.

Jambo hili limeleta picha mbaya mbele ya mashabiki wa soka na hata wachezaji wa zamani, ambao wamewashauri kuchukua hatua sahihi ili kujiondoa katika picha mbaya wanayoonekana sasa mbele ya jamii.

Harry Redknapp, kocha wa zamani wa Tottenham na Portsmouth, ameiambia BBC: “Nimefadhaishwa kwa kweli, wanautumia mpango wa serikali vibaya. Watumishi hawa ni muhimu kwa kila klabu, klabu hazipaswi kuchukua pesa ya serikali kuwalipa hawa.

“Wachezaji wanapaswa kufanya mikutano baina yao na kutokea mioyoni mwao waseme ‘nadhani hili ni wazo zuri, hebu tukatwe sisi mishahara yetu’, pesa ziongezwe kwa watumishi hawa, lakini hilo litoke mioyoni mwao kabisa.

“Serikali ilipoanzisha mpango huu wa kuwasaidia wenye vipato vya chini ililenga biashara ambazo hazimudu kubaki na wafanyakazi (zilifikiria kuwapunguza), na nadhani haikulenga kutumia pesa za walipakodi kuzisaidia klabu za Ligi Kuu ya England ambazo zinamudu kuwalipa mamilioni mastaa wao kila wiki.”

Mchambuzi maarufu wa soka katika gazeti Daily Mail, na shabiki mkubwa wa Arsenal, Piers Morgan alisema: “Ni kituko kwa klabu yoyote ya soka kukata mishahara ya watumishi wake, lakini inaendelea kuwalipa kifahari wachezaji wake.”

Kufikia sasa, hakuna klabu ya Ligi Kuu ya England ambayo imekata mishahara ya wachezaji wake kutokana na janga la virusi vya corona ambalo limeshakuchua maisha ya watu 2,352 nchini Uingereza.

Gordon Taylor, mwenyekiti Mtendaji wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), ambaye anaingiza Pauni 2 milioni kwa mwaka amewataka wachezaji kutokubali kukatwa mishahara yao, huku Ligi Kuu ya England ikitarajia kufanya mkutano wa dharura leo kuamua hatima yao.