Corona kuikwamisha Raja kuifuata Zamalek Misri

Johannesburg, Afrika Kusini (AFP). Klabu ya Raja Casablanca ya Morocco imesema haitaweza kusafiri kwenda Misri kucheza na Zamalek katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwishoni mwa wiki baada ya wachezaji wake wanane kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Mechi hiyo imepangwa kufanyika Jumamosi katika Uwanja wa International jijini Cairo baada ya Raja kufungwa bao 1-0 nyumbani nchini Morocco katika mechi ya kwanza iliyofanyika Jumapili iliyopita.
"Mamlaka za Morocco zimefuta kibali kilichotolewa kwa klabu cha kusafiri nje ya nchi," kiongozi mmoja aliiambia AFP leo Jumatano.  
Wachezaji wanne wa Raja waliokuwa katika kikosi kilichoanza dhidi ya Zamalek Jumapili-- beki Ilias Haddad, viungo Omar Arjoune na Mouhcine Moutouali, na mshambuliaji Abdelilah Hafidi ni miongoni mwa waliogundulika kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.
Vyombo vya habari vya Morocco pia vilimtaja kiungo Abderrahim Achchakir na washambuliaji Anas Jabroun, Ayoub Nanah na Mohamed Zrida kuwa ni miongoni mwa waliopata maambukizi.   
Shangwe zilizoibuka mwezi huu baada ya Raja kutwaa ubingwa wa Morocco kwa mara ya kwanza katika miaka saba zinahusishwa na maambukizi hayo.