Conte anavyobeba mastaa kuizima Juve Italia

Muktasari:

Na Kocha Antonio Conte baada ya kutua tu Inter, kitu chake cha kwanza alichopania ni kumaliza ubabe wa Juventus kwenye kubeba taji la Serie A kwa misimu kibao mfululizo.

MILAN, ITALIA . CHEKI msimamo wa Serie A unavyosomeka. Juventus ipo kileleni ikiwa imekusanya pointi 51 baada ya mechi 21. Chini yake, kwenye nafasi ya chini ipo Inter Milan, iliyokusanya pointi 48 baada ya kushuka uwanjani mara 21.

Kwenye mechi hizo, Juve imeshinda 16 na Inter 14 huku Juve ikitoka sare mara tatu na kuchapwa mbili, wakati Inter imetoka sare mara sita na kuchapwa mara moja. Timu hizo zimetofautiana pointi tatu tu.
Na Kocha Antonio Conte baada ya kutua tu Inter, kitu chake cha kwanza alichopania ni kumaliza ubabe wa Juventus kwenye kubeba taji la Serie A kwa misimu kibao mfululizo.
Katika kulimaliza hilo, Conte, anayependeleza zaidi kutumia fomesheni ya 3-5-2 amevamia kwenye Ligi Kuu England na kunasa mastaa kadhaa akiamini watakwenda kumaliza ubabe wa Juventus.
"Ukimwondoa Diego Godin, wachezaji wengine wote hawajashinda kitu, hawana uzoefu," alisema Conte.
Katika kuhakikisha anashusha wazoefu kwenye kikosi chake, Conte amevamia kwenye Ligi Kuu England na kwenda kuwanasa mastaa kadhaa ambao mwenye anaamini wakitua katika kikosi chake watakuja kuifanya kuwa ya kiushindani zaidi, ambapo alivamia Manchester United akawanasa mastaa watatu, washambuliaji Romelu Lukaku na Alexis Sanchez (mkopo) kisha akamchukua beki wa pembeni, Ashley Young. Conte amemnasa pia staa mwingine aliyetamba kwenye Ligi Kuu England, Victor Moses, ambaye alikuwa naye huko Chelsea na kwenye dirisha la Januari, amevamia Tottenham Hotspur kwenda kumnyakua kiungo Christian Eriksen.
Na sasa Conte kikosi chake cha kwanza huko Inter akitumia mfumo wa 3-5-2, golini ni Handanovic, atakayelindwa na ukuta wa mabeki watatu, De Vrij, Godin na Young na kwenye kiungo kutakuwa na mastaa watano, Vecino, Eriksen, Sensi, Moses na Sanchez na kwenye fowadi ni Lukaku na Martinez.