Comoro yaiduwaza Misri yapaa kileleni Kundi G Afcon 2021

Muktasari:

Comoro inaongoza Kundi G ikiwa na pointi nne ikifuatiwa na Misri na Kenya zenye pointi mbili kila moja na Togo ina pointi moja.

Cairo, Misri. Comoro imewaduwaza watu kwa kuongoza Kundi G na kuwaacha Misri, Kenya na Togo wakipigana vikumbo katika kampeni ya kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2021 Cameroon.

Comoro imekuwa na matokeo ya kushangaza mwaka huu baada ya kuifunga Togo kabla ya kulazimisha suluhu na Misri na hivyo kufikisha pointi nne ikifuatiwa na Misri na Misri zenye pointi mbili kila moja na Togo ya mwisho.

Comoro iliwaduwaza mabingwa wakihistoria Misri kwa kulazimisha suluhu nyumbani ikiwa ni rekodi yao nzuri zaidi dhidi ya miamba hiyo ya Afrika.

Hata hivyo Comoro wamebebwa na sare 1-1 waliyopata Kenya na Togo katika mchezo mwingine wa kundi hilo.

Kenya pia ilifanikiwa kupata pointi moja ugenini dhidi ya Misri katika mchezo uliochezwa siku chache zilizopita katika ufunguzi wa mashindano hayo.

Johannah Omollo alifunga bao la kuongoza kwa Kenya ‘Harambee Stars’ katika kipindi cha kwanza kabla ya Togo kusawazisha kupitia Hakim Ouro-Sama.