Coastal Union yatua kibabe Dar ikiwasubiri KMC

Muktasari:

 

  • Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema, mchezaji wake Ali Kiba  ataungana na wenzake baada ya kumalizika mchezo huo kwa safari ya Tanga kwani huko wana michezo mitatu mfululizo.

Dar es Salaam. Klabu ya Coastal Union ya Tanga imewasili jijini Dar es Salaam asubuhi leo Jumanne kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC utakaopigwa Alhamisi hii  Uwanja wa Uhuru.

Kocha wao mkuu, Juma Mgunda, ameliambia MCL Digital kuwa anatambua ugumu wa mchezo huo lakini hayupo tayati kupoteza mechi za ugenini mfululizo.

"KMC wamekuwa na matokeo mazuri wanapokuwa wapo nyumbani kwao na hilo nalijua, hata hivyo sisi pia hatutaki kupoteza tena kwa hiyo mchezo utakuwa mzuri na tutapambana kuona tunashinda," alisema Mgunda.

Kocha huyo mwenye mwili mkubwa aliongeza kwa kusema kuwa katika dirisha dogo la usajili hajasajili sehemu kubwa ya wachezaji kwa sababu anawaamini vijana wake alioanza nao msimu.

"Matokeo tu ya mpito tumeyapata lakini wachezaji wangu wanacheza kitimu, hawa ni vijana wa leo, kesho na kesho kutwa kwa hiyo bado tunajenga timu ambayo itakuwa ya muda mrefu," alisema Mgunda ambaye ni mchezaji wa zamani wa Coastal.