Coastal Union, Lyon hapatoshi Uhuru saa 10 hii

Friday September 14 2018

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema wapo tayari kuikabili African Lyon leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Saa 10 jioni.

Coastal ipo nafasi ya sita katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi tano itacheza mechi yake ya kwanza ugenini tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kucheza michezo mitatu mfululizo nyumbani huku ikishinda mmoja na kutoa sare michezo miwili.

Mgunda alisema wanazitaka pointi tatu za ugenini kwani wamepania msimu huu kupata ushindi kila sehemu.

"Msimu huu tumejipanga kupata ushindi kila sehemu, hatuangalii tuko nyumbani au ugenini.

"African Lyon ni timu nzuri ina wachezaji wazuri hivyo haitakuwa mechi rahisi kwetu. Muhimu ni kupambana zaidi ili kuweza kupata matokeo," alisema Mgunda.

Naye mshambuliaji wa kigeni wa African Lyon, Mfaransa Victor da Costa amesema kwa maandalizi waliyoyafanya anaamini watapata ushindi wao wa kwanza msimu huu dhidi ya Coastal Union.

African Lyon imecheza mechi tatu na kuambulia pointi mbili kwa kutoka sare michezo miwili na kupoteza mmoja.

Victor da Costa alisema wamefanya maandalizi mazuri kipindi ligi iliposimama na mchezo mmoja wa kirafiki waliocheza dhidi ya Yanga hivi karibuni umekijenga kikosi chao.

“Yanga walitupa kipimo kizuri kuelekea mchezo wa Ijumaa (dhidi ya Coastal Union), naamini tupo tayari na tutaanza kuwashangaza wengi. Natambua kuwa Lyon sio timu kubwa hapa nchini lakini ina wachezaji wenye uwezo wa kupambana na kupata matokeo ya ushindi.

“Binafsi nina maelewano mazuri na Boban ambaye nimekuwa nikicheza naye, kuna muda huwa anashuka chini nabaki mwenyewe na akiona nina mpira husogea kwa haraka ili  kutoa msaada, tunacheza kwa kupokezena, hiyo ni mbinu ambayo itatusaidia,” alisema mshambuliaji huyo.

Advertisement