Chuji afichua siri yake

Thursday August 9 2018

 

By THOMAS NG’ITU

KIUNGO Athuman Idd ‘Chuji’ anayekipiga katika klabu ya Coastal Union, amekuwa akiwashangaza watu wengi namna ambavyo anakuwa anaelewana na wachezaji pamoja  na mashabiki wengi wa soka.

Mchezaji huyo aliyewahi kuichezea Yanga, aliliambia Mwanaspoti kwamba amekuwa akijishusha kwa kila mtu ili kuhakikisha kwamba sehemu yoyote anayokuwa anapata heshima yake ile ile.

“Watu wengi hawapendi kujishusha unajua na hilo linaweza likafanya hata usipate timu, kuna muda inabidi ukubali kwamba kuna maisha yalipita na yamekuja mengine, kwahiyo mimi niko sawa na kila mtu inawezekana ndio mana hata katika mpira bado nipo,” alisema.

Akizungumzia kikosi chao ambapo yeye ndiye mkongwe katika timu hiyo, alisema kwamba timu yao ina vijana wengi ambao wanataka kutengeneza historia zao za mpira.

“Kikosi chetu kweli kina wachezaji vijana lakini hawa ndio hawa wazuri kwasababu nao wanataka kufanya vizuri, lakini sisi pia tupo nina imani tutafanya vizuri katika msimu ujao,” alisema.

Chuji ni miongoni mwa wachezaji wazoefu wanaoingoza msimu huu timu hiyo katika Ligi Kuu, akiwa na kipa Hussein Sharifu ‘Casilas’, ambaye naye aliwahi kuichezea Simba.