Chobanga aitaka nafasi ya Simba

Wednesday May 15 2019

 

By Bertha Ismail

ARUSHA.TIMU ya Alliance Queens ya jijini Mwanza baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya soka la wanawake uliotwaliwa na JKT, sasa inataka kumaliza katika nafasi ya pili inayoshikiliwa na klabu ya Simba Queens kwa sasa.

Chobanga ameyasema hayo jijini Arusha baada ya kuwanyeshea mvua ya mabao 6-1 timu ya Tanzanite Queens ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

“Ubingwa wa ligi hii tumeukosa kwa sababu mbalimbali zilizokuwa nje ya uwezo wetu ambazo naamini mwakani uongozi wa klabu utafanyia kazi ikiwamo suala la udhamini wa timu na uchumi kwa ujumla. JKT wameshachukua ubingwa lakini nafasi ya pili ndiyo naitaka nitoke nafasi ya tatu niliyopo sasa. Narudi nyumbani kujipanga kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mapinduzi ya Njombe kwenye Uwanja wa Nyamagana,” alisema.

“Msimu ujao tunaomba pia ratiba ziboreshwe kwani ratiba ya msimu huu si rafiki. Unakuta mechi mbili katikati ya wiki na wanaocheza ni watoto wa kike tena bila kupumzika. Hilo likizingatiwa, mambo yatakuwa sawa pia wadhamini nao waongeze kiwango kidogo cha pesa,” aliongeza Chobanga.

Naye kocha mkuu wa Tanzanite Abdalah Juma alisema kiujumla wamepoteza nyumbani kutokana na mapungufu yaliyojitokeza na hivi sasa wanajipanga kuelekea Dodoma kucheza dhidi ya Baobao Queens mchezo wa mwisho kumaliza ligi.

Aidha hadi sasa timu ya Alliance iko nafasi ya tatu kwa alama 44 walizofungana na timu ya Simba Queen’s walioko nafasi ya pili wakitofautishwa na mabao ya kufunga na kufungwa, huku kinara wa ligi hii akisimama JKT Queen’s kwa alama 63.

Advertisement

Timu ya Evergreen wameshuka hadi Daraja la Kwanza kwa kuwa na alama 10.

Advertisement