Chirwa akiwasha Azam mapema unambiwa

Muktasari:

Chirwa amejiunga na Azam hivi karibuni akiungana na kocha wake wa zamani wa Yanga, Pluijm na mshambuliaji mwenzake Donald Ngoma.

Dar es Salaam.Mshambuliaji mpya wa Azam, Obrey Chirwa leo asubuhi ameanza kujifua kwa mara ya kwanza na kikosi cha mabingwa hao wa Kombe la Chalenji kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga amejiunga na Azam kama mchezaji huru baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na klabu ya Nagoon ya Misri.

Hata hivyo Chirwa itabidi asubiri hadi dirisha dogo litakapofungiliwa ili kuthibitisha usajili wake kabla ya kuanza kuitumikia timu yake mpya.

Mchezaji huyo alionekana mwenye furaha wakati wa mazoezi hayo yaliyofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi ambapo timu hiyo inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi Ruvu Shooting utakaofanyika Novemba 22.

Kocha mkuu wa Azam, Hans Pluijm aliwapa mazoezi makali wachezaji wake akiwa na lengo la kurudisha ufiti kwa wachezaji baada ya mapumziko ya takribani siku sita.

Chirwa amejiunga na Azam hivi karibuni akiungana na kocha wake wa zamani wa Yanga, Pluijm na mchezaji mwenzake Donald Ngoma.

Mazoezi ya Azam yalihudhuriwa na wachezaji wote isipokuwa  wale wealioitwa timu zao za Taifa wakiwemo Aggrey Moris, Abdallah Kheri, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’,Yahya Zayd (wote Taifa Stars) na Nickolas Wadada ambaye yuko katika kambi ya Uganda Cranes 

Azam inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza michezo 12, imeshinda mechi tisa na kutoa sare mitatu huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote.