Chirwa 'kujiunga' Simba

Muktasari:

Mzambia Obrey Chirwa kuhusishwa kwenda Simba, Popat amesema si jambo la kushtua kwa kuwa maisha ya soka ni mafupi na mchezaji anaangalia kwenye maslahi mazuri.

KLABU ya Azam FC ipo katika hekaheka ya kuhakikisha inawabakiza nyota wake ambao, mikataba inaelekea mwishoni kumalizika.
Lakini, katika kuhakikisha hilo linatimia wameanza kumalizana na Donald Ngoma kwa kumpa mkataba mpya, baada ya kuonyesha kiwango bora zaidi.
Hata hivyo, vigogo wa Azam wameanza kuingiwa na hofu kwa straika wao mpya Obrey Chirwa, ambaye ameonekana kuwa mgumu kusaini dili jipya.
Mwanaspoti limedokeza kuwa, Chirwa amekuwa akisita kusaini mkataba mpya kutokana na kutovutiwa na ofa ya Azam huku Simba wakiwa mlangoni wakifuatilia kinachoendelea.
Habari zilizopatikana zinaeleza kwamba, Simba iko tayari kutoa dau la Sh 85 milioni ili kumsainisha Chirwa mkataba wa miaka miwili.
Chanzo hicho kimeeleza zaidi kwamba, mazungumzo ya Chirwa na Simba yalianza kwa siri, lakini hajafikia uamuzi wa kusaini dili hilo kutokana na kuombwa kupokea fedha nusu kwanza.
“Chirwa anaweza kuondoka kwa na ofa aliyopewa Simba, ila anahofia kupewa pesa nusu ya usajili wakati huku Azam anaweza kupewa kamili,” alisema.
Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ kuzungumzia ishu ya Chirwa kugomea mkataba mpya, ambapo alisema walikaa kujadiliana na hakuna makubaliano yaliyofikiwa mpaka sasa.
Hata hivyo, amesema kuwa bado wanaendelea kumshawishi kuona kama ataendelea kubaki klabuni hapo.
“Chirwa alisaini miezi sita na tulikuwa katika majadiliano ya kuongeza mkataba, lakini hatujaafikiana. Bado tunaendelea kuzungumza na tukifikia mwafaka basi atasaini na lolote linaweza kutokea,” alisema.
Kuhusu Chirwa kuhusishwa kwenda Simba, Popat alisema sio jambo la kushtua kwa kuwa maisha ya soka ni mafupi na mchezaji anaangalia kwenye maslahi mazuri.
“Wachezaji wanaangalia maisha ya baadaye, soka sio kazi kama kazi zingine huku ukicheza ni miaka 10, hivyo kama kuna ofa kubwa nje ya Azam anaweza kuchagua,” alisema Popat.