Chipukizi wa Tanzania kuwasha moto Sweden, Norway

Muktasari:

Mashindano hayo ya kimataifa ambayo yatafanyika katika miji ya Oslo, Norway na Gothenburg, Sweden majira haya ya kiangazi barani Ulaya pia yamelenga kuwakutanisha watoto pamoja na kufurahi.

Dar es Salaam. Kituo cha Magnet Youth Sports Organisation (MYSO), kimetoa timu nne za vijana Kwenda Sweden na Norway kwaajili ya kushiriki kombe la Gothia na Norway.

Mwenyekiti wa kituo hicho, Tuntufye Mwambu alisema wanaenda kushindana nchini humo kutokana na uzoefu waliona wa kushiriki mashindano mbalimbali ya vijana.

"Timu inasafiri leo na kesho kwa makundi tofauti, tutaanza Sweden ambako kunamashindano ya Gothia ambayo yataanza Julai 14 hadi 20, baada ya hapo ni Norway.

"Norway kwenyewe ni katika kombe la Norway na lenyewe ni la vijana, hii sio mara yetu ya kwanza, misimu iliyopita tulienda na kufika mbali hivyo safari ni imani yetu kuwa tutafanya vizuri zaidi, " alisema Tuntufye.

Miongoni mwa timu hizo zinazosafiri ya kwanza ni vijana chini ya umri wa miaka 11, mbili ni vijana chini ya umri wa miaka 12 wakiwa na viongozi wao.

Mwenyekiti wa kituo hicho, alitoa shukrani zake kwa shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF na Serikali kwa kuwaunga mkono katika juhudi zao za kuwaendeleza vijana.

Kwa niaba ya TFF, mkurugenzi wa fedha na utawala wa shirikisho hilo, Cornel Barnabas alisema wataendelea kushirikiana na vijana hao huko waendako.

"Niliongea na vijana wanaonekana wanaweza kufanya vizuri kwa namna walivyojiandaa, nawatakia kila la kheri na bila shaka wataipeperusha vema bendera ya Tanzania, " alisema.