Wenger: Chipukizi hawawezi kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Manchester United

Muktasari:

Wenger anaamini kwamba wachezaji vijana wa United kama Scott McTominay, Mason Greenwood na Daniel James hawajajiandaa kuwa wachezaji wa kuanza katika klabu kubwa kama ya Manchester United na itakuwa ngumu kwao kupata mafanikio.

London, England. Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger alifahamika kuwa muumini wa wachezaji vijana ametoa kali kwa kumwambia kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer hawezi kutwaa ubingwa Ligi Kuu England akiwa na wachezaji chipukizi.

Manchester United imeanza ovyo msimu huu ikishinda mechi moja, kutoka sare mbili na kufungwa moja, na tayari Wenger anaamini Man United haina wachezaji waliopevuka vya kutosha kuweza kupata mafanikio msimu huu.

Wenger ameweka wazi kuwa kikosi hiki ni tofauti na kile kizazi cha Manchester United cha mwaka 1992 maarufu kama Class of ’92 ambacho kilipandishwa kutoka kikosi cha vijana na kocha maarufu wa zamani, Sir Alex Ferguson na kupata mafanikio makubwa kwa kipindi kirefu.

Wenger anaamini kwamba wachezaji vijana wa United kama Scott McTominay, Mason Greenwood na Daniel James hawajajiandaa kuwa wachezaji wa kuanza katika klabu kubwa kama ya Manchester United na itakuwa ngumu kwao kupata mafanikio.

 “Unapoona unajua kuwa ni mmoja kati ya mfano wa sehemu ambapo kuna vipaji lakini bado hawajajua kucheza kwa pamoja. Labda hawa wachezaji hawajapevuka vya kutosha kuweza kuibeba timu kama Manchester United,” alisema Wenger.

“Wanaweza kufuata nyayo za kile akina (Ryan) Giggs, (Paul) Scholes, (David) Beckham walichofanya kwa miaka mingi? Binafsi sijashawishika kabisa.” Alisema kocha huyo Mfaransa ambaye aliachana na Arsenal Mei 2017.

Solskjaer alikuwa staa wa zamani wa klabu hiyo amepunguza wastani wa umri kwa wachezaji wake huku akiwatumia zaidi Mason Greenwood (17), Aaron Wan-Bissaka, Daniel James, Marcus Rashford (wote 21), Scott McTominay (22) na Andreas Pereira (23).