Breaking News
 

Chipukizi Azam apania kulipa kisasi kwa URA

Friday January 12 2018

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Azam, Shaban Iddi amesema mchezo wa kesho wa fainali dhidi ya URA utakuwa wa kisasi, katika kuhakikisha wanatetea ubingwa wao.

Azam watakuana na URA kesho kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Idd alisema anaamini yeye pamoja na wachezaji wenzake watapambana na kufanya vizuri katika mchezo huo na kuhakikisha kombe linabaki Azam.

“Itakuwa mechi ngumu kwani URA si timu rahisi na kumbuka walitufunga katika hatua ya makundi hivyo na sisi lazima tulipe kisasi."

 "Tunaweza kuchukua ubingwa kama kila mmoja atapambana na tukashirikiana. Sisi ni timu bora na naamini tutafanikisha malengo yetu katika mchezo huo"alisema Idd.

Azam ilitinga fainali baada ya kuichapa Singida United bao 1-0 lililofungwa na Idd.

Mchezaji huyo amerejea kwa kasi katika kikosi hicho baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu akifunga katika mchezo dhidi ya Simba, Azam waliposhinda bao  1-0 na dhidi ya Singida United.

 “Naishukuru Azam kwa kunitibia vizuri mpaka nimepona na kurudi uwanjani. Licha ya kwamba sichezi dakika nyingi kutokana na ,ripoti ya daktari inavyotaka, lakini nashukuru hata dakika hizo chache nimeweza kuzitumia vizuri na naamini kama nitakuwa fiti basi nitafunga zaidi,"alisema Iddi.