Chipsi yai funga ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Saturday April 13 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND

MECHI za kwanza za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imepigwa wiki hii inayoisha na hakika lilipigwa soka la kiwango kikubwa sana. Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wote walikuwa mzigoni kutafuta matokeo kwa timu zao huku mechi hizo zikiacha kumbukumbu kibao ambazo hakika ungependa ufungashiwe na kuondoka nazo. Haya hapa mambo manane yaliyoibuka baada ya hizo mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizochezwa Jumanne na Jumatano ya wiki inayomalizika, ambapo Liverpool wao walijipigia FC Porto, Tottenham Hotspur waliichapa Manchester City, huku Juventus wakitoka sare na Ajax na Manchester United wakipigwa nyumbani Old Trafford na Barcelona. Hii hapa take-away ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

8. Lloris ni mfalme wa penalti

Kipa, Hugo Lloris wa Tottenham Hotspur ameokoa penalti tatu ilizokabiliana nazo timu yake katika michuano tofauti ndani ya mwaka huu wa 2019. Kipa huyo namba moja wa Ufaransa, ameokoa penalti kwenye mechi dhidi ya Leicester City, Arsenal na Manchester City tangu mwaka huu ulipoanza. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne aliokoa penalti ya Sergio Aguero.

7. Klopp ashinda mechi 400

Ushindi iliyopata Liverpool mbele ya FC Porto walipowachapa 2-0, kocha Mjerumani, Jurgen Klopp ylikuwa ushindi wake wa 400 tangu alipoanza kujishughulisha na ukocha. Katika ushindi hio, Klopp ameshuhudia Liverpool ikishinda mara 111, wakati kwenye kikosi cha Borussia Dortimund alishinda mara 180 na kwenye kikosi cha Mainz 05 chama lake hilo akiwa kocha hapo lilishinda mechi 109.

6. Tottenham wazee wa faida

Rekodi ziko hivi, Tottenham Hotspur imevuka kwenye hatua zote zilizofuatia kw enye Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tisa tofauti matukio ambayo walishinda mechi zao za kwanza za hatua ya mtoano. Jumanne iliyopita, Spurs waliichapa Man City 1-0 shukrani kwa bao la Heung-min Son na kama wataendeleza rekodi zao basi wababe hao ni wazee wa faida, wanaposhinda mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano, basi ni lazima wasonge mbele. Wamefanya hivyo mara tisa.

5. Suarez apiga mechi 50

Straika, Luis Suarez amekuwa mchezaji wa tano wa kutoka taifa la Uruguay aliyefikisha mechi 50 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Diego Godin na Edinson Cavani wao kila mmoja amecheza mechi 59, wakati Maxi Pereira na Paolo Montero kila mmoja amecheza mechi 57. Mchezo wake wa Old Trafford ambapo mpira wake wa kichwa ulimfanya Luke Shaw ajifunge, hiyo ilikuwa mechi ya 50 kwa Suarez kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

4. Man United balaa kwa kujifunga

Manchester United waliruhusu bao jingine la kujifunga kwenye mchezo wao wa kwanza wa hatua ya robo fainali waliocheza na Barcelona Jumatano iliyopita huko Old Trafford na kuchapwa 1-0. Na sasa Man United imefikisha mabao manane ya kujifunga kwenye michuano hiyo, hakuna timu nyingine iliyojifunga mara nyingi hivyo kwenye historia ya ligi hiyo na kufanya taji la kutikisa nyavu lishikiliwe na Man U.

3. Man United yaweka rekodi chafu

Kwenye mchezo wao dhidi ya Barcelona, Manchester United ilishindwa kupiga hata shuti moja golini wakichapwa 1-0 na jambo hilo limewafanya kuandika rekodi chafu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu Machi 2005. Hiyo Machi 2005, Man United walicheza mechi yote bila ya kupiga shuti hata moja golini kwa mpinzani wao na wakicheza na AC Milan.

2. Barca yaipiga Man United viwanja vinne tofauti

Barcelona imejipigia Manchester United katika viwanja vinne tofauti kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwenye mechi zao, Barca wameichapa Man United uwanjani Nou Camp, Stadio Olimpico, Wembley na Old Trafford. Kwenye viwanja vya Stadio Olimpico na Wembley walikutana kwenye mechi za fainali za michuano hiyo ya Ulaya na mara zote wachezaji waliotikisa nyavu zao ni Messi.

1. CR7 anafunga tu robo fainali

Cristiano Ronaldo anafunga mabao yake pale inapohitajika kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Supastaa huyo wa Ureno anayekipiga Juventus msimu huu, Jumatano alifunga kwa kichwa kwenye sare ya 1-1 ugenini kwa Ajax. Jambo hilo limemfanya Ronaldo kufikisha mabao 24 kwenye mechi 21 alizocheza robo fainali Ulaya, huku Messi akiwa amefunga mara 10 tu. Kwa ujumla amefunga mara 125 katika mechi 161 za Ulaya.

Advertisement