Chilunda, Morris wampoteza Kagere, Azam bingwa

Muktasari:

  • Bingwa wa mashindano ya Kombe Kagame amejinyakulia dola 30,000

Dar es Salaam. Mabao ya Shabaan Chilunda, Aggrey Morris kuwafanya mabingwa watetezi wa Azam FC kutetea ubingwa wao kwa kuichapa Simba 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Chilunda alifunga bao la kuongoza dakika 32, akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Bruce Kangwa kufanya timu hizo kwenda mapumziko matokeo yakiwa Azam 1-0 Simba.

Kipindi cha pili Simba ilirudi kwa kasi na dakika 63, mshambuliaji wake mkongwe Meddie Kagere ilisawazisha bao hilo akiunganisha pasi nzuri ya Said Ndemla.

Furaha hiyo ya Simba haikudumu muda mrefu dakika 68, Morris aliifungia Azam bao la pili kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa wa Simba, Deogratius Munisi ‘Dida’. Faulo hiyo ilitokea baada ya Pascal Wawa kumchezea vibaya Chilunda nje ya eneo la 18.

Azam iliendelea kutawala mchezo huo na dakika 87,  ilipata penalti baada ya beki wa Simba, Mohamed Hussein kumchezea vibaya mchezaji wa Azam kwenye eneo la hatari, lakini kipa Razack Abaloa alipoteza nafasi hiyo kwa kupaisha penalti hiyo.

Ubingwa huo ni ishara njema kwa kocha Hans Pluijm aliyeanza maisha yake mapya katika kikosi cha Azam.

Katika mchezo huo mashabiki wa Simba walijitokeza kwa wingi kuliko wa Azam ambao baadhi wamevalia jezi za Yanga na wengine mavazi ya kawaida.

Vigoma na miruzi na kelele za hapa na pale kutoka jukwaa la mashabiki wa Simba na Azam FC vinasikika kila kona ya uwanja.