Chelsea noma sana !

Muktasari:

  • Mabao ya Pedri na Ruben Loftus-Cheek waliofunga katika kila kipindi yalitosha kuifanya Chelsea kufikisha pointi 31 zilizokuwa zikiwapandisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo kabla ya mechi ya mahasimu wengine wa huko London, Arsenal na Spurs kumenyana jioni ya jana

LONDON, ENGLAND.CHELSEA imerudi kwenye makali yake ya kugawa vipigo kwenye Ligi Kuu England baada ya jana Jumamosi kuipiga Fulham Mbili Bila huko Stamford Bridge.

Wababe hao wanaofahamika kama The Blues walihitaji ushindi huo kuweka mambo yao sawa kwenye ligi hiyo baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo.

Chelsea ilitoka sare ya bila kufunga na Everton kabla ya kwenda kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Tottenham Hotspur huko Wembley, lakini matokeo ya jana yamerudisha matumaini ya Kocha Maurizio Sarri katika kuufukuzia ubingwa wa msimu huu.

Mabao ya Pedri na Ruben Loftus-Cheek waliofunga katika kila kipindi yalitosha kuifanya Chelsea kufikisha pointi 31 zilizokuwa zikiwapandisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo kabla ya mechi ya mahasimu wengine wa huko London, Arsenal na Spurs kumenyana jioni ya jana. Mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu zimekuwa tamu kweli kweli kutokana na vigogo kuzidi kuchuana kwenye mchakamchaka huo.

Manchester City inaoongoza kwa kukusanya pointi 38 katika mechi 14 ilizocheza, wakati Liverpool ikishika nafasi ya mbili na pointi zao 33, lakini hiyo ilikuwa kabla ya mechi yake ya jana dhidi ya Everton kwenye Merseyside derby huko Anfield.

Kigogo pekee ambaye anapumulia mashine kwenye ligi hiyo kwa msimu huu ni Manchester United, ambayo imekusanya pointi 22 tu katika mechi 14 ilizocheza, huku ikiwa imeshinda mara sita tu, sare nne na vichapo vinne.

Kuhusu Chelsea kwenye mechi yake hiyo ilionekana kuwa na dhamira ya kushinda baada ya kupiga mashuti tisa golini, wakati Fulham yenyewe ilikomea mashuti manne tu.

Kocha Sarri hakuwa na wakati mgumu akishuhudia timu yake ikitawala mchezo kwa muda mrefu, ikimiliki mpira kwa asilimia 67. Mechi hiyo ilimshuhudia Kocha Claudio Ranieri akirejea Stamford Bridge kuwakabili waajiri wake hao wa zamani, lakini mambo hayakuwa mazuri kwa upande wake akikumbana na kipigo ambacho kinaifanya Fulham kuzidi kuburuza mkia kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi nane tu ilizobeba katika mechi 14 ilizocheza. Fulham msimu huu imepata ushindi mara mbili tu kwenye ligi hiyo na kutoka sare mara mbili, huku kipigo hicho kutoka kwa Chelsea kikiwa cha 10 kwake na kuiweka kwenye hatari ya kushuka daraja.